Osha yatoboa siri uchumi wa viwanda

27Jun 2016
Ashton Balaigwa
Morogoro
Nipashe
Osha yatoboa siri uchumi wa viwanda

TANZANIA inaweza kufanikiwa katika mkakati wake wa kukuza uchumi wa viwanda ikiwa Serikali itahakikisha inasimamia na kutekelezwa kwa sheria ya afya na usalama mahali pa kazi.

Meneja wa Wakala wa Afya na Usalama Mahali pa Kazi (Osha) Kanda ya Mashariki, Jerome Materu

Hayo yalielezwa na Meneja wa Wakala wa Afya na Usalama Mahali pa Kazi (Osha) Kanda ya Mashariki, Jerome Materu, wakati akifunga mafunzo ya afya na usalama mahali pa kazi yaliyoshirikisha makampuni 56 ya uzalishaji na utoaji huduma kutoka mikoa ya Dar es Salaam, Pwani na Morogoro.

Alisema kuifanya nchi kuwa ni ya uchumi wa viwanda ni moja ya mikakati ya Rais John Magufuli na kwamba ili viwanda viweze kuzalisha kwa tija, lazima sheria ya afya na usalama mahali pa kazi ya mwaka 2003 isimamiwe na kutekelezwa kikamilifu.

Alisema sheria hiyo inataka kila kiwanda ama kampuni ya uzalishaji na utoaji huduma kuhakikisha inaunda kamati za afya ili ziweze kutoa huduma za kwanza na kutoa elimu ya namna ya kufanyakazi katika mazingira salama.

Alisema kamati hizo zinasaidia kwa kiasi kikubwa kupunguza ajali, majanga na magonjwa yanayotokana na kazi kwani zimekuwa zikitoa elimu ya matumizi ya vitendea kazi, huduma ya kwanza na namna ya kujiokoa wakati yanapotokea majanga maeneo ya kazi.

Materu aliwataka waajiri wa makampuni, viwanda na maeneo mengine ya kazi kuunda kamati hizo kwani Osha itafanya ukaguzi na kuwachukulia hatua kali za kisheria waajili watakaoshindwa kuunda kamati hizo ikiwa ni pamoja na kuwatoza faini isiyopungua Sh. milioni mbili.

Mwezeshaji wa mafunzo ya huduma ya kwanza kutoka Osha, Hans Mpela, alisema wafanyakazi wengi wamekuwa wakipoteza maisha ama kupata ulemavu wa kudumu kutokana na kukosa huduma ya kwanza wanapopata ajali ama majanga katika maeneo ya kazi.

“Mfanyakazi anaweza kupoteza fahamu kutokana na kusimama muda mrefu kama hatapatiwa huduma ya kwanza anaweza kupoteza maisha ama kupata tatizo kubwa la kiafya, hivyo mafunzo haya ni muhimu sana,” alisema Mpela.

Baadhi ya washiriki wa mafunzo hayo walisema mara kadhaa wamekuwa wakishuhudia ajali na magonjwa mbalimbali kikiwamo Kifua kikuu (TB) kwa wafanyakazi wenzao kutokana na kufanyakazi katika mazingira yasiyozingatia afya na usalama, hivyo kupoteza maisha ama kupata ulemavu wa kudumu.

Mmoja wa washiriki hao kutoka kampuni ya kutengeneza maji ya kunywa ya Udzungwa, Frank Bangimoto, alisema kampuni nyingi zimejikuta ziliingia gharama kubwa ya kuwatibia na kuwalipa fidia wafanyakazi wanaopata magonjwa ama ajali kwenye maeneo yao ya kazi.

www.guardian.co.tz/circulation

Habari Kubwa