Pikipiki kutaifishwa kisa magendo ya kahawa

05Jul 2019
Lilian Lugakingira
KARAGWE
Nipashe
Pikipiki kutaifishwa kisa magendo ya kahawa

SERIKALI ya Wilaya ya Karagwe mkoani Kagera, imewaonya vijana wanaosafirisha abiria kwa kutumia bodaboda, kuacha tabia ya kuvusha kahawa kimagendo kwenda Uganda kwa kutumia bodaboda hizo.

Imesema watakaokamatwa pikipiki zao zitataifishwa, watachukuliwa hatua za kisheria ikiwamo kufikishwa mahakamani.

Onyo hilo lilitolewa na Mkuu wa Wilaya hiyo, Godfrey Mheruka, wakati wa kukabidhi pikipiki 22 zenye thamani ya zaidi ya shilingi milioni 270 zilizotolewa kwa waendesha bodaboda wilayani humo, kupitia chama cha kuweka na kukopa cha umoja wa vijana Karagwe, kilichoanzishwa mwaka 2009 na aliyekuwa Mwenyekiti wa Umoja wa Vijana wa Chama Cha Mapinduzi (UVCCM) mkoa wa Kagera, Yahaya Kateme.

Mheruka alisema mbali na kuvusha kahawa kimagendo, pia baadhi yao wanafaulisha viroba vya pombe na maeneo yanajulikana ikiwamo la Kihanga, na kuwa wote watakamatwa na kuwajibishwa kwa mujibu wa sheria.

“Hata wale mnaovusha kahawa kwa magendo baadhi yenu tunawajua, lakini mfahamu kufanya hivyo mnawaathiri wazee wenu, mnaiba kahawa kwenye miti, mnaweka kwenye magunia na kwenda kuuza kimagendo Uganda, ole wenu ikikamatwa pikipiki yoyote inafanya magendo ya kahawa, mhusika atakwenda rumande, pikipiki na kahawa vinataifishwa na serikali,” alisema.

Alisema kuwa serikali haitakuwa tayari kuwavumilia watu wa namna hiyo, na kuwataka vijana waliokopeshwa pikipiki hizo kufanya kazi halali na kwa bidii ili waweze kurejesha kwa wakati na kuwezesha wenzao ambao hawajapata fursa hiyo kukopa.

Kwa upande wake mwanzilishi wa SACCOS hiyo ya vijana Yahya Kateme alisema kuwa kabla ya kuanzisha mradi huo wa “Kijana miliki pikipiki yako” walifanya utafiti na kugundua kuwa vijana walio wengi wanaendesha pikipiki za mabosi na kutakiwa kurejesha shilingi 10,000 kwa siku, na kuwa kupitia mradi huo vijana watamiliki pikipiki zao.

“Malengo makubwa ya Saccos hii ni kuwainua vijana kiuchumi, kwa hiyo tuliona ni bora kijana akakopeshwa pikipiki, na atakapomaliza mkopo inakuwa ya kwake na anaweza kuitumia kufanya shughuli nyingine,” alisema Kateme.

Naye Mhasibu Msaidizi wa Saccos hiyo, Johaiven John, alisema tangu kuanzishwa kwake wameshatoa mikopo kwa vijana yenye thamani ya zaidi ya shilingi bilioni mbili.