Pilipili manga ni kipaumbele’

08Nov 2019
Na Mwandishi Wetu
Dodoma
Nipashe
Pilipili manga ni kipaumbele’

NAIBU Waziri wa Kilimo, Hussein Bashe, amesema pilipili manga ni miongoni mwa mazao ya bustani yanayoendelea kupewa
umuhimu wa kuzalishwa nchini kutokana na mahitaji yake kama
kiungo na dawa za binadamu.


Bashe aliyasema hayo wakati alipokuwa akijibu swali la
Mbunge wa Muheza (CCM), Balozi, Adadi Rajabu, ambaye alitaka
kujua mpango wa serikali wa kutuma wataalamu kubaini ni kwa nini zao hilo
limeshuka thamani.


Pia alitaka kujua serikali ina mpango gani wa kuwasaidia wakulima
hao ili waweze kulima kilimo cha kisasa.


“Wananchi wa Tarafa ya Amani wamelima zao la pilipili manga kwa wingi, hivi karibuni bei ya zao hilo imeanguka sana kutoka Sh.12,000 hadi Sh. 4,000, jambo linalowaumiza sana wakulima,” alisema Rajabu.


Bashe alisema pilipili manga ni miongoni mwa mazao ya bustani
yanayoendelea kupewa umuhimu wa kuzalishwa nchini
kutokana na mahitaji yake kama kiungo na dawa za binadamu.


Alisema, kutokana na umuhimu huo, Machi 2019, serikali ilituma
wataalamu kufanya tathmini ya hali ya uzalishaji wa mazao ya viungo
ikiwamo pilipili manga kwenye Halmashauri za Wilaya ya Muheza na
Morogoro.


“Tathmini ilibaini kwamba bei ya pilipili manga imeshuka kutoka Sh.
13,000 kwa kilo mwaka 2017 hadi Sh. 4,500 kwa kilo katika mwaka
2019 sawa na asilimia 20 kutokana na ongezeko la uzalishaji kwa zao
hili nchini pamoja na nchi wazalishaji wakubwa ambao ni Vietnam,
Indonesia, Srilanka, Brazili na India,” alisema Bashe.


Alisema uzalishaji wa ndani wa zao hilo uliongezeka kutoka tani
7,836.40 mwaka 2014/2015 hadi tani 12,318.3 mwaka 2017/2018.
Alisema uzalishaji duniani kwa mwaka 2017 ulifikia tani 725,000 ikilinganishwa na mahitaji yanayokadiriwa kuwa tani 400,000 kwa mwaka.