Pinda ataka PASS Trust kujitangaza

24Jul 2021
Renatha Msungu
Dodoma
Nipashe
Pinda ataka PASS Trust kujitangaza

WAZIRI Mkuu Mstaafu, Mizengo Pinda, ameitaka Taasisi ya PASS TRUST kutumia wiki yao ya maonyesho kuwatembelea wakulima wa maeneo mbalimbali ili kujitangaza shughuli wanazofanya.

Pinda aliyasema hayo jana wakati akifungua wiki hiyo inayofanyika katika Viwanja vya Nyerere Square jijini hapa.

Alisema wakulima wengi hivi sasa hawaijui PASS inafanya nini dhidi yao, hivyo ni vyema katika wiki hii kutumia nafasi hiyo kujitangaza ili wajasiriamali wakulima kuwatambua na kutumia fursa ya kupata mikopo.

"Nawaomba mtumie hii wiki kutoa elimu ya utambuzi kwa wakulima,kwa sababu wengi hawawajui,"alisema Pinda.

Alisema wakulima wengi hawajui taasisi hiyo inafanya nini na kwamba wakiwatembelea wakulima pembezoni basi itawasaidia kujitambulisha kwa wajasiriamali ambao ni wakukima na kuwaeleza nini wanafanya na wao watajitokeza kupata fursa za kilimo.

Aliwapongeza kutokana na kujikita katika kusaidia wajasiriamali kwenye shughuli za kilimo.

Alisema jitihada wanazofanya kusaidia serikali kuwekeza katika sekta ya kilimo zinapaswa kuendelezwa na kuungwa mkono ili kuwasaidia wakulima.

Mwenyekiti wa Bodi ya PASS, Dk. Tausi Kida, alisema taasisi hiyo ipo bega kwa bega na sekta ya kilimo ndiyo maana wameanzisha wiki ya PASS ili kutoa elimu kwa wajasiriamali.

Dk. Kida alisema lengo lake ni kuona wakulima wanaufaika na huduma zinazotolewa na taasisi hiyo katika maeneo mbalimbali hapa nchini lengo ikiwa ni kuinua sekta ya kilimo.

Alisema taasisi yao inajishughulisha na wakulima wadogo, wakubwa na wa kati hivyo wanapaswa kuchangamkia fursa ya mikopo ambayo inatolewa na PASS Leasing ili kuinua kilimo chao cha kila siku.