Posho ya mil. 1/- ya meya kukirimu wageni kila sikukuu yafutwa

08Sep 2016
John Ngunge
Arusha
Nipashe
Posho ya mil. 1/- ya meya kukirimu wageni kila sikukuu yafutwa

MKURUGENZI mtendaji wa Halmashauri ya Jiji la Arusha, Athumani Kihamia, amefuta posho ya Sh. 1,000,000 iliyokuwa ikitolewa kwa meya kama motisha, kukirimu wageni nyumbani kwake kila siku za sikukuu.

Alisema posho hiyo ilipitishwa na Baraza la Madiwani, lakini haikupata kibali cha Tamisemi, hivyo ilikuwa ikitolewa kinyume cha sheria na kanuni.

Akizungumzia uamuzi huo mbele ya kikao cha Baraza la Madiwani, Kihamia alisema posho hiyo ilikuwa ikitolewa kinyume
cha sheria.

Kihamia ambaye aliteuliwa na Rais John Magufuli kuwa Mkurugenzi wa Jiji la Arusha, Julai mwaka huu, alisema alikuta posho hizo zikiwa zinatolewa kwa meya na mkurugenzi wa jiji kila siku za sikukuu kama motisha.

Aliwataka viongozi na madiwani kuwa wavumilivu wakati huu wa mabadiliko ya kikanuni kuhusu malipo ya fedha yaliyokuwa nje ya utaratibu na kamwe hawezi kuyaruhusu kuendelea kulipwa hata kama yaliidhinishwa katika utaratibu ambao ni kinyume cha kanuni.

Alisema posho ya malipo ya Sh. 1,000,000 kwa meya na ile aliyokuwa akipata mkurugenzi kwa kila sikukuu na malipo ya Sh. 500,000 kwa jili ya posho ya safari hayapo katika kanuni ya fedha za Tamisemi.

Alisema hapaswi kulipwa kiasi hicho cha fedha anapotoka nje ya mkoa kwa sababu kanuni ya 81(a)-(e) hakielezi wala kuidhinisha malipo hayo.

Alisema amefuta malipo hayo yaliyokuwa yakitolewa kwake na meya na kwamba wote wanapaswa kujitegemea kuwakirimu wageni kwa kutumia mishahara na marupurupu mengine yanayoruhusiwa kwa mujibu wa kanuni.

Aidha, amefuta posho ya mafuta ya Sh. 100,000 iliyokuwa ikitolewa kwa madiwani kila mwezi, posho ya vocha ya simu kwa ajili ya muda wa maongezi ya Sh. 150,000 kila mwezi kwa kila diwani.

Pia amefuta nyongeza ya nauli kutoka 60,000 hadi 80,000 na kuirudisha hadi Sh. 10,000 inayotolewa kwa kwa ajili ya kuwawezesha kuhudhuria vikao vya mabaraza.

Alisema posho hizo zilikuwa zikitolewa kinyume cha kanuni za Tamisemi.

Aidha, ameanza kuwakata fedha za posho za simu walizokuwa wakilipwa kuanzia Novemba mwaka jana, makato ambayo yalianza kutekelezwa Agosti, mwaka huu.