PPRA: Wananchi changamkieni fursa ya zabuni kwa mtandao

05Jul 2019
Na Mwandishi Wetu
Dar es Salaam
Nipashe
PPRA: Wananchi changamkieni fursa ya zabuni kwa mtandao

MAMLAKA ya Udhibiti wa Manunuzi ya Umma (PPRA), imewataka wananchi kuendelea kutembelea banda lao katika Maonyesho ya 43 ya Kimataifa ya Biashara maarufu kama Sabasaba yanayofanyika jijini Dar es Salaam, ili kupata elimu ya sheria na Mfumo wa Manunuzi kwa Njia ya Mtandao (TANePS).

Afisa Mtendaji Mkuu wa PPRA, Mhandisi Leonard Kapongo akizungumza na wafanyakazi wa Mamlaka hiyo kwenye Maonesho ya 43 ya Kimataifa ya Biashara.

Ofisa Mtendaji Mkuu wa PPRA, Mhandisi Leonard Kapongo ambaye alikuwa kwenye banda hilo, aliwaambia waandishi wa habari kuwa mamlaka inaendelea kusimamia Sheria ya Manunuzi ya Umma ya Mwaka 2011 iliyofanyiwa marekebisho mwaka 2016, ili kuhakikisha kuwa manunuzi yanayofanywa yanazingatia thamani halisi ya fedha.

Aidha, aliwataka wananchi kushirikiana na mamlaka kutoa taarifa kuhusu ukiukwaji wa Sheria ya Manunuzi ya Umma na kwamba wahusika watachukuliwa hatua.

Mhandisi Kapongo alisema kuwa uzingatiaji wa Sheria ya Manunuzi ya Umma ni nyenzo ya kudhibiti matumizi ya fedha za umma katika kuhakikisha kuwa fedha zilizotolewa kwa ajili ya maendeleo zinatumika kama zilivyokusudiwa ili kufikia malengo ya kuwa nchi yenye uchumi wa kati na kuboresha maisha ya Watanzania.

Katika maonyesho hayo, PPRA inatoa elimu kuhusu Mfumo wa Manunuzi ya Umma kwa Njia ya Mtandao (TANePS), ambao unalenga katika kuongeza uwezo na uwajibikaji katika michakato ya manunuzi nchini.

Kwa mujibu wa mamlaka hiyo, wazabuni 1,958 wameshajiandikisha katika TANePS. Wazabuni hao ni kutoka katika mikoa mitano iliyofanyiwa majaribio katika Mwaka wa Fedha 2018/19. Mikoa hiyo ni Dar es Salaam, Dodoma, Arusha, Mwanza na Mbeya.

Mfumo unawezesha manunuzi ya bidhaa, kazi za kandarasi, ushauri wa kitaalamu, na ushauri usio wa kitaalamu pamoja na uunzaji wa mali za serikali kwa njia ya tenda.

TANePS ilizinduliwa rasmi Juni mwaka 2018 ambapo watoa huduma waliagizwa kujisajili katika mfumo huo ili kupata fursa ya kushiriki fursa za manunuzi ya umma kwa njia ya mtandao.

Habari Kubwa