Rais Brazil katika kashfa ya rushwa

22Sep 2016
Na Mwandishi Wetu
Nipashe
Rais Brazil katika kashfa ya rushwa

RAIS wa zamani wa Brazil, Luiz Inacio Lula da Silva, anatarajia kufikishwa mahakamani kwa tuhuma za rushwa na utakatishaji fedha zinazoihusisha kampuni ya tasifa ya mafuta ya Petrobras.

Hati ya mashtaka inadai kwamba Lula alikubali kupokea dola milioni 1.11 (zaidi ya Sh. bilioni 2.2) katika mradi wa mabilioni ya dola.

Wakati mashtaka hayo yakiwa tayari, kiongozi huyo pia alishtakiwa Agosti, mwaka huu, kwa madai ya kuingilia uchunguzi. Hata hivyo amekanusha madai hayo yote na kudai kuwa ni ya kisiasa zaidi.

"Ninasikikitika sana. Ni mambo ya kizushi na yameegemea kisiasa zaidi. Kinachoendelea ni kujaribu kunichafua mbele ya wananchi hasa wafuasi wangu na jamii ya kimataifa kwa ujumla,” alisema.

Jaji Sergio Moro, ambaye anasimamia uchunguzi kuhusu madai ya Petrobras, maarufu kama ‘Operation Car Wash’, alisema kuna ushahidi wa kutosha juu ya Lula kuhusika katika kashfa hiyo.

Kwa mujibu wa hati ya mashtaka inayomkabili rais huyo wa zamani, fedha anazodaiwa kuzipokea alizitumia kwa ajili ya kununua na kukarabati nyumba ya kifahari ufukweni.

Nyumba hiyo ya ghorofa ilijengwa na kampuni moja ya ujenzi ambayo pia imehusishwa katika kashfa hiyo. Sambamba na kampuni hiyo, mke wa Lula, Marisa Leticia, na watu wengine sita pia wamehusishwa.
Lula ametuhumiwa na waendesha mashtaka kuwa kinara wa mpango huo ambao umeigharimu kampuni zaidi ya dola bilioni mbili (zaidi ya Sh. trilioni nne).

Katika kashfa hiyo inayomhusu Lula na familia yake, wanasiasa na viongozi wa juu kadhaa wa Petrobras wamekamatwa na wengine kufungwa baada ya uchunguzi uliochukua takriban miaka miwili.
Wachunguzi wanaamini kwamba fedha nyingi kuliko uhalisia zilizolipwa kwa makandarasi kupitia Petrobras zilitolewa kwa misingi ya rushwa.

Kwa mujibu wa madai hayo ya wachunguzi, baadhi ya fedha hizo zilitumika katika kugharimia kampeni za uchaguzi kusaidia vigogo kadhaa, Lula akiwamo.

Lula, ambaye alikuwa rais wa Brazil kati ya mwaka 2003 na 2011, ni mmoja wa viongozi mashuhuri na anaelezwa kuwa anaweza kuwa mgombea wa urais wa nchi hiyo katika uchjaguzi mkuu wa mwaka 2018.

Hata hivyo, umaarufu wa chama chake cha wafanyakazi umeporomoka baada ya kung’olewa kwa mrithi wake, Dilma Rousseff, mwezi uliopita.
Kashfa hiyo ya rushwa huenda ikamzuia Lula kugombea urais katika uchaguzi ujao.

Habari Kubwa