Rais Mwinyi awaonya watendaji udhalilishaji

30Jul 2021
Rahma Suleiman
Zanzibar
Nipashe
Rais Mwinyi awaonya watendaji udhalilishaji

RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Hussein Ali Mwinyi, amesema hatasita kumchukulia hatua mtendaji yeyote aliyemteua, akibainika kujihusisha na vitendo vya udhalilishaji.

Dk. Hussein Ali Mwinyi.

Alitoa onyo hilo jana katika kongamano la harakati za kutokomeza vitendo vya udhalilishaji Zanzibar lililofanyika Kikwajuni mjini Unguja.

Dk. Mwinyi alisema haitakuwa rahisi kwake kumvumilia kiongozi anayeendekeza udhalilishaji na kurudisha nyuma mapambano dhidi ya vitendo hivyo.

"Jambo linalonisikitisha sana kwamba wateule ninaowateua nao naambiwa wanajihusisha na udhalilishaji, niwaambie wananchi kwamba nimefanya kimakosa na nikibaini kwamba yupo mtendaji ambaye anafanya mambo haya, sitasita kumchukulia hatua,” alihadharisha.

Alisema umefika wakati sasa kujipanga upya katika kupambana na vitendo vya udhalilishaji nchini kwa ngazi zote zinazohusiana na kushughulikia mambo hayo.

“Ukiyasikia haya yanayosemwa hapa mimi binafsi napata huzuni kubwa kwa sababu inaonekana taasisi zinazotakiwa kufanya kazi zao hazifanyi na zina watu wanajulikana lakini wapo wanaendelea kutizamwa bila ya kuchukuliwa hatua,” alisema.

Rais Mwinyi alisisitiza umefika wakati kila mtu kwa nafasi yake ajitathmini na kuwataka viongozi waliokuwa chini yake kutoa taarifa kwa yale yote yaliyozungumzwa na wananchi katika kongamano hilo.

Dk. Mwinyi alisema yeye kama kiongozi wa nchi atakuwa mstari wa mbele katika kulifanikisha jambo hilo ili vitendo vya udhalilishaji vinaondoka nchini.

Alisema anatafakari wakati umefika kuanzisha mamlaka ya kupinga vitendo vya udhalilishaji kama mamlaka ya kudhibiti dawa za kulevya ili kuipa mamlaka uwezo wa kufanya mambo yake yenyewe ikiwamo kuchunguza kesi na kupeleka mahakamani.

“Wapo wanaume ambao wanawapiga wake zao halafu wakija mnaawaambia kawaida tu, lakini dini zinatwambia unapotaka kumpiga mke basi upo utaratibu unaotuelekeza,” alisema.

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Katiba Sheria, Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Haroun Ali Suleiman, alisema vitendo vya udhalilishaji vinaumiza sana.

Alisema serikali ya awamu ya saba iliunda kamati ya kitaifa ya kushughulikia mambo hayo, lakini bado vyombo vinavyoshughulikia mambo hayo havipo makini katika kushughulikia matendo ya udhalilishaji.

Mkurugenzi kutoka Jumuiya ya Wanasheria Wanawake Zanzibar (ZAFELA), Jamila Mahmoud, alisema kongamano hilo lina lengo la kupima asasi za kiraia katika kuondosha udhalilishaji.

Alisema kwa mwaka uliopita, ZAFELA ilipokea kesi 100 na kwamba kuanzia Januari hadi Juni mwaka huu, wamepokea malalamiko mapya 887 huku kituo cha huduma cha sheria kikipokea kesi zaidi ya 50 za watoto kukinzana na sheria.

Katika kongamano hilo Rais Mwinyi alizindua mfumo wa kukusanya takwimu sahihi za mapambano dhidi ya udhalilishaji nchini.

Habari Kubwa