Rais wa AfDB aipongeza Tanzania ukuaji uchumi

17May 2019
Na Mwandishi Wetu
Nipashe
Rais wa AfDB aipongeza Tanzania ukuaji uchumi

RAIS wa Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB), Dk. Akinwumi Adesina, ameipongeza Tanzania kwa ukuaji mzuri wa uchumi wa wastani wa asilimia saba kwa mwaka na hivyo kuendelea kuwa miongoni mwa nchi zenye uchumi unaokua kwa kasi kubwa duniani.

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli akimkabidhi zawadi ya picha ya Wanyama Rais wa Benki ya Maendeleo ya Afrika AfDB Dk. Akinwumi Adesina.

Dk. Adesina alitoa pongezi hizo jana Ikulu jijini Dar es Salaam muda mfupi baada ya kukutana na kufanya mazungumzo na Rais Dk. John Magufuli kuhusu ushirikiano kati ya benki hiyo na Tanzania katika maeneo mbalimbali ya maendeleo.

Dk. Adesina alimpongeza Rais Magufuli kwa dhamira yake njema na msimamo wake wa kuwapigania Watanzania na alimtaka aendelee na mwelekeo huo ambao umeendelea kuimarisha uchumi kwa ukuaji wa wastani wa asilimia saba ikilinganishwa na wastani wa ukuaji wa uchumi wa dunia wa asilimia 3.5.

Alimpongeza kwa ushirikiano na nchi jirani kama vile Uganda na hivyo kufanikisha ujenzi wa mradi mkubwa wa bomba la kusafirisha mafuta ghafi lenye urefu wa kilometa 1,443 kati ya Hoima nchini Uganda na Bandari ya Tanga nchini kwa kushirikisha sekta binafsi.

Aidha, Dk. Adesina alisema wamezungumzia kuhusu kilimo na kwamba AfDB ipo tayari kusaidia kutatua tatizo la masoko ya mazao yanayozalishwa katika kanda mbalimbali za Tanzania na kuongeza thamani.

Kuhusu miradi mingine ya maendeleo alisema kwa hivi sasa AfDB imetoa ufadhili kwa miradi yenye thamani ya Sh. trilioni 4.55 na kwamba hivi karibuni benki hiyo imeidhinisha ufadhili kwa miradi ya ujenzi wa barabara za mzunguko (ring road) za Jiji la Dodoma zenye urefu wa kilometa 110.

Alisema fedha zingine ni za ujenzi wa Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Msalato mkoani Dodoma na pia aliipongeza Tanzania kwa kuanza mradi mkubwa wa ujenzi wa reli ya kati kwa kiwango cha kisasa kati ya Dar es Salaam na Dodoma kwa kutumia fedha zake na ameahidi kuwa benki hiyo itaunga mkono mradi huo hasa kwa ujenzi wa kuanzia Isaka kwenda Kigali nchini Rwanda na kunufaisha nchi nyingine za Burundi na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo.

Kwa upande wake, Rais Magufuli alimshukuru Dk. Adesina kwa ushirikiano mkubwa ambao AfDB inautoa kwa Tanzania na amemhakikishia kuwa Tanzania itahakikishia fedha zinazotolewa na benki hiyo zinatekeleza miradi iliyokusudiwa kwa uhakika na inaleta matokeo yanayotarajiwa.

Rais Magufuli alisema pamoja na miradi hiyo AfDB pia imekubali kutoa fedha kwa ajili ya ujenzi wa barabara ya lami ya Mpanda – Tabora yenye urefu wa kilometa 359, kujenga awamu ya pili ya mradi wa miundombinu ya mabasi yaendayo haraka (BRT) kati ya Kariakoo na Mbagala jijini Dar es Salaam na kujenga njia ya umeme ya msongo wa kilovoti 400 kati ya Sumbawanga – Mpanda – Kigoma – Nyakanazi.

Kuhusu AfDB kusaidia ujenzi wa reli ya kati kwa kipande cha kuanzia Isaka mpaka Kigali, Rais Magufuli alisema ufadhili huo utasaidia kuharakisha usafirishaji wa madini yaliyopo katika kanda ya kati na magharibi mwa Tanzania.

Habari Kubwa