RAS awataka wahitimu misitu kujituma

21Nov 2020
Francis Godwin
Iringa
Nipashe
RAS awataka wahitimu misitu kujituma

KATIBU  Tawala  wa Mkoa wa Iringa, Hapinnes Seneda, amewataka   wahitimu  wa Chuo  cha Viwanda vya Misitu (FITI), kuhakikisha  wanajituma   zaidi katika utendaji kazi   ili  kuongeza thamani ya mazao ya  misitu  kwa   kuzalisha samani zenye ubora.

Kwa kufanya hivyo, Seneda amesema taifa litaachana na utegemezi wa samani kutoka nje ya nchi.

Akizungumza  juzi na   wahitimu wa FITI   na  uongozi  wa Taasisi ya  Uendelezaji Misitu  Tanzania (FDT), Seneda alisema serikali imeendelea  kuboresha mazingira ya  uwekezaji  wa  viwanda  mbalimbali  vikiwamo  vya uchakataji  wa mazao ya  misitu, hivyo   kupitia  chuo  hicho, ni  wazi  watapatikana   wataalamu  zaidi  wa  kuongeza thamani ya mazao ya  misitu.

Seneda alisema Iringa ni  moja ya mikoa yenye  utajiri  mkubwa wa  miti, hivyo iwapo   wahitimu hao watajituma katika  kutumia elimu  waliyopata kwa  kujitika zaidi katika kuongeza thamani ya mazao ya  misitu kwa kutengeneza samani zenye ubora, ni  wazi soko la bidhaa zao litaongezeka  zaidi.

Aliwataka  wahitimu hao   kwenda  kufanya kazi  kwa  bidii  na  kuachana na tabia  ya kutanguliza maslahi  zaidi  badala ya  kuonyesha  ubora  wa kazi katika maeneo ambayo wanakwenda  kufanya kazi kwa  kujitolea.

Kupitia  mafunzo ambayo  wamepata, alisema wahitimu  hao  wana uwezo  mkubwa wa kuongeza  ujuzi katika  kazi ili  kutengeneza bidhaa za  kisasa  zitokanazo na mazao ya  misitu.

Kwa mujibu wa Katibu Tawala, sababu ya watu kukimbilia  kununua bidhaa za  nje  ni  ubora  uliopo kwenye  bidhaa  hizo lakini kama  vijana  na  wawekezaji wa ndani  wataboresha  bidhaa  zao, hakutakuwa na ulazima wa  kuagiza samani kutoka nje.

Alisema   serikali imekuwa  ikitoa  mikopo  kwa  vijana  kupitia Halmashauri  ili  kuwawezesha wale waliojiunga katika makundi  kuongeza mitaji katika  shughuli  zao japo  si rahisi kwa   serikali  kutoa  mikopo kwa  watu  ambao hawaonyeshi  wanafanya  nini.

Pia  alisema   hata   kupitia  taasisi  za  kifedha,  mikopo  ipo lakini lazima kuwapo na andiko kutoka kwa  waombaji  ambalo   linaonyesha  shughuli wanayofanya au wanayotaka kufanya.
Seneda aliipongeza FDT kwa   jitihada  mbali mbali  inazoendelea  kufanya katika  mkoa wa Iringa  kuona mazingira yanaendelea  kuboreshwa  kwa  kupanda miti   zaidi pia kuonyesha  fursa  zitokanazo na  mazao ya  misitu katika kuwakomboa wananchi wengi hasa  wale  wanaojishughulisha na kilimo cha miti .

Mkurugenzi Mtendaji wa FDT, David Shambwe,  alisema  ofisi yake  imeendelea   kupata   ushirikiano mkubwa   kutoka  ofisi ya  mkuu  wa  mkoa na  tayari  wamezungumza na wenye  viwanda vya mazao ya  miti na kupeana elimu mbalimbali .

Shambwe alisema  programu  hiyo ni moja ya  chachu  kubwa kwa vijana na  uendelezaji  wa viwanda vyenye   ubora  nchini  hasa katika mazao ya misitu iwapo  wadau  mbalimbali  wataunga  mkono .

Habari Kubwa