Rasilimali mifugo kulipia mfuko wa afya

14Nov 2017
Mohab Dominick
Nipashe
Rasilimali mifugo kulipia mfuko wa afya

WAZEE katika Halmashauri ya Ushetu, wilayani Kahama wametakiwa kutumia rasilimali ya mifugo yao kuiuza ili kupata fedha ya kulipita Mfuko wa Afya  ya Jamii (CHF) iliyoboreshwa.

 Alisema moja ya changamoto inawakabili wananchi wa Halmashauri ya Ushetu hususani kundi la wazee kujiunga na CHF ni pamoja na kusahau kuwa wana rasilimali ya mifugo ambayo inaweza ikawasadia kulipia matibabu.

Mkurugenzi wa Halmashauri ya Ushetu, Michael Matomora, alisema hayo katika kikao baina ya Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga, Zainab Telack, aliyekuwa katika ziara ya siku moja ya kuhamasisha wananchi kujiunga na mfuko huo.

Matomora alisema, Halmashauri ya Ushetu ina watu 3, 522 ambao hawajaingizwa katika mfumo rasmi huku kaya 859 zikiwa zimeingizwa katika mapango wa CHF.

Mkurugenzi alisema halmashauri ya Ushetu ina zaidi ya wazee 8,000 huku wengi wakidhani kuwa ni masikini wakati wana rasilimali kubwa ya mifugo kama ng’ombe wanao weza kuuza na kupata fedha ya kulipia mfuko huo.

“Nashangaa wazee wengi katika Halmashauri ya Ushetu wanadhani kuwa wao ni masikini huku wakisahau kuwa wamezungukwa na mifugo, wanaweza kuuza na kupata fedha kwa ajili ya kulipia mfuko huo wa afya ya jamii na kuwasaidia wao pamoja na wategemezi watano,” alisema.

Alisema kwa sasa halmashauri yake imeanza kazi ya kuwatambua wazee hao ikiwa ni pamoja na kuwapa elimu ya kutambua utajiri walionao huku lengo kubwa likiwa ni kuhamasisha wananchi wengi kujiunga na CHF iliyoboreshwa.

Meneja wa Mradi wa Tuimarishe Afya (HPSS), Mkoa wa Shinyanga Dk. Harun Kasale, alisema kwa sasa halmashauri za Mkoa wa Shinyanga hazina budi kuwarudisha wanachama walionekana kujitoa katika mfuko katika kipindi kilichopita kutokana na sababu mbalimbali.

Kasale alisema, mkoa wa Shinyanga una jumla ya wanachama 29,000 na kuongeza hadi kufikia Desemba 30, wanatarajia kuandikisha zaidi ya asilimia 30 ya wanachama.

Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga, Zainab Telack, alisema lazima wanachama wengi waingie kwa hiari na kumtaka mkurugenzi huyo kuwahamasisha wakulima wa tumbaku kujiunga watakapopata fedha zao za mauzo.

“Lazima katika zahanati zetu pamoja na vituo vya tuwe na nembo ya CHF pamoja na daftari kwa ajili ya kuwaorodhesha wanachama wetu na pia tutakuwa na dawati la kukaa wagonjwa pamoja na kabati lenye nembo kwa ajili ya kuwapa kipaumble wanachama wote waliojiunga na mfuko huo,” alisema.