RC aishukia kampuni ununuzi tumbaku madai ya wakulima

26Nov 2021
Nebart Msokwa
Chunya
Nipashe
RC aishukia kampuni ununuzi tumbaku madai ya wakulima

MKUU wa Mkoa wa Mbeya, Juma Homera, ameijia juu kampuni ya ununuzi wa tumbaku ya MO Green International Ltd kutokana na kuchukua tumbaku ya wakulima wilayani Chunya bila kuwalipa zaidi ya Sh. milioni 460.

Ameitaka kampuni hiyo kulipa fedha hizo kabla ya Aprili, mwakani na kwamba alitaka aanze kuishughulikia sasa hivi lakini akabaini kwamba kuna makubaliano ambayo kampuni hiyo imeingia na wakulima kuwa italipa ikifika wakati huo.

Homera alionyesha kukerwa na kampuni hiyo alipofanya ziara ya kuwatembelea wakulima wa tumbaku wilayani hapa kwa ajili ya kukagua maandalizi ya msimu mpya, kukagua vitalu vya miche ya miti iliyoandaliwa na kufungua ghala la kuhifadhia tumbaku la Chama cha Msingi cha Igagwe (AMCOS).

Alisema endapo kampuni hiyo haitalipa fedha hizo ifikapo Aprili, atalichukulia hatua za kisheria kwa kuwa imesababisha hasara kwa wakulima ikiwa ni pamoja na kukwamisha kilimo cha zao hilo.

Mkuu wa mkoa alisema alishawahi kukutana na malalamiko ya wakulima wa mkoa wa Katavi alipokuwa mkuu wa mkoa huo wakiilalamikia kampuni hiyo kuwa ilichukua tumbaku yao bila kuwalipa na kwamba alifuatilia mpaka wakalipwa.

“Hawa lazima nishughulike nao. Wakitaka wakimbie nchini na hata wakifanya hivyo tutafuatilia kwenye ubalozi wao mpaka fedha hizo zote zilipwe. Nawaomba wakulima endeleeni kuvuta subira mpaka mwezi huo ambao viongozi wamekubaliana halafu wasilipe waone,” alisema Homera.

Aliitaka Bodi ya Tumbaku Tanzania kuhakikisha inawapelekea wakulima wa tumbaku wanunuzi wa uhakika kwa kufuatilia historia yao kuanzia nchi wanakotoka na uzoefu wao kwenye ununuzi wa zao hilo kwenye mataifa mengine.

Awali, Ofisa Ushirika kutoka Tume ya Maendeleo ya Ushirika Tanzania, Mkoa wa Mbeya, Biezery Malila, alisema mbali na kampuni hiyo kudaiwa na wakulima pia inadaiwa ushuru na Chama Kikuu cha Ushirika wa Wakulima wa Tumbaku (CHUTCU) pamoja na vyama vya msingi.

Alisema mpaka sasa kampuni hiyo inadaiwa Dola za Kimarekani 39,660.21 ambazo ni za vyama vya msingi vya Kalangali, Nkung’ungu, Malangali, Mapinduzi pamoja na CHUTCU.

Kitendo cha kampuni hiyo kuchelewa kuwalipa wakulima hao, alisema kimekuwa na athari kwa wakulima ikiwamo kushindwa kuandaa mashamba kwa ajili ya msimu wa kilimo ujao kutokana na kutokuwa na fedha za kuwalipa vibarua.

Pia alisema baadhi ya wakulima wameshindwa kuwapeleka watoto wao shule kutokana na kukosa fedha kwa ajili ya ada na kwamba wengine wameshinda kulipa madeni waliyokuwa wanadaiwa wakati wa kuandaa mashamba msimu uliopita.

Alisema tatizo hilo limesababisha vyama vya msingi kushindwa kujiendesha kwa kushindwa kuwalipa wafanyakazi ambao vimewaajiri kwenye ofisi zao.

“Baada ya kuona tatizo hili limekuwa kubwa tuliamua kumshirikisha Mkuu wa Wilaya ambaye ametusaidia mpaka sasa kampuni hiyo imeshawalipa wakulima Dola 907,515.50 kati ya Dola milioni 1.16 na baada ya kulipa fedha hizo ndipo waliahidi kumalizia mwezi Aprili,” alisema Malila.

Mkuu wa Wilaya ya Chunya, Mayeka Simon, alisema ofisi yake imekuwa ikishirikiana na wakulima kufuatilia fedha hizo na kwamba alibaini kuwa kampuni hiyo haina mtaji wa kutosha kufanya biashara ya tumbaku.

Alisema ili kuondokana na tatizo hilo Bodi ya Tumbaku inatakiwa kufuatilia kwa kina kampuni zinazonunua tumbaku ili kuepuka migogoro isiyokuwa ya msingi kwa madai kuwa mpaka sasa kuna migogoro kati ya wakulima na viongozi wa vyama vyao vya msingi.

Habari Kubwa