RC aitaka taasisi kufanya utafiti udongo

17Jun 2021
Grace Mwakalinga
Ileje
Nipashe
RC aitaka taasisi kufanya utafiti udongo

MKUU wa Wilaya ya Ileje, James Mkude, ameiomba Taasisi ya One Acre Fund,  inayojihusisha na utoaji huduma za kilimo na pembejeo, kuanza utafiti wa udongo ili kuwasaidia wakulima kujua aina gani ya mbegu na wakati sahihi wa kulima mazao mbadala kama vile karanga na alizeti ambayo mavuno yake ni-

-mengi ikilinganishwa na mengine.

Mkude alisema hayo jana wakati wa siku ya uvunaji iliyofanyika katika Kata ya Mbebe na kuhudhuriwa na zaidi ya wakulima 220 na viongozi mbalimbali.

Alisema utafiti wa udongo utawasaidia wakulima kulima kwa tija kupitia wataalamu wa kilimo ambao watashauri namna bora ya kulima mazao mbadala ambayo kwa sasa hayajapewa kipaumbele.

"Mazao kama vile karanga na alizeti hapa Ileje yanakubali sana. Nimeona  wakulima wanapata mavuno mengi, nashauri tujielekeze huko maana faida ipo, One Acre Fund mtusaidie kutoa elimu ya ugani na masoko ya uhakika, serikali iko nyuma yenu," alisema Mkude.

Mkude aliwahamasisha wakulima kujiunga kwenye vyama vya ushirika ili kuwa na uamuzi wa pamoja katika uuuzaji wa mazao yao hususani mahindi ambayo kwa sasa soko lake limedorora.

Alimwomba Ofisa Ugani Mkoa wa Songwe kufanya kikao na maofisa ugani wa wilaya zote za Songwe kuweka mikakati ya kutoa elimu juu ya faida za vyama vya ushirika.

Kaimu Mtendaji wa Kijiji cha Mbebe, Mwinuka Mtwangi, alisema mazao ya kimkakati yanafaida kubwa kuliko mazao mengine kama vile mahindi, hivyo aliiomba One Acre Fund kuweka kipaumbele.

Aliongeza kuwa karanga na alizeti kwa debe moja huuzwa kuanzia Sh. 7,000 hadi 8,000 wakati mahindi huuzwa Sh. 4000 kwa debe.

Alisema wateja wa alizeti na karanga ni wa uhakika na kwamba wakiongezewa ujuzi watalima eneo kubwa na kwa ufanisi huku akiiomba taasisi hiyo kuendelea kutoa mbegu bora na za uhakika zinazokidhi mahitaji ya soko la ndani na nje ya nchi.

Habari Kubwa