RC akemea makundi ndani ya ushirika

06Mar 2021
Shaban Njia
Kahama
Nipashe
RC akemea makundi ndani ya ushirika

MKUU wa Mkoa wa Shinyanga, Zainab Telack, ameitaka bodi mpya ya Chama Kikuu cha Ushirika Kahama (KACU), kuacha makundi yasiyo na tija katika utekelezaji wa majukumu yao.

Amesema makundi huwagawa wakulima wa tumbaku na pamba na kwamba hatua hiyo husababisha mpasuko ndani ya ushirika.

Telack alisema hayo juzi muda mfupi baada ya kukamilika kwa uchaguzi wa bodi mpya na mwenyekiti wa chama hicho, Emmanuel Charahani.

Alisema kuna tabia ya baadhi ya viongozi wa bodi kuendekeza makundi baada ya uchaguzi kukamilika, hivyo kuwagawa wakulima na kusababisha migogoro isiyo na tija.

Kutokana na tabia hiyo, alisema serikali haitasita kuwawajibisha kisheria watakaobainika kutengeneza makundi ndani ya ushirika.

“Ushirika huu umekuwa mfano wa kuigwa nchi nzima katika kutetea maslahi ya wakulima na kujiendesha kwa faida. Nikiwa mlezi wa ushirika, sitakubali mharibikiwe ndani ya uongozi wangu kwa kulea tabia za baadhi ya viongozi wachache wasiokuwa wadilifu,” alisema Telack.

Pia alisema taasisi za kifedha zimekiamini chama hicho na kukikopesha fedha ambazo zitawanufaisha wakulima wote wa pamba na tumbaku na kwamba kutengeneza makundi kutasababisha kupoteza imani kwa taasisi hizo na kushindwa kuendelea kukopesheka.

Naye Mrajisi Msaidizi wa Vyama vya Ushirika Mkoa wa Shinyanga, Hilda Boniphace, alisema sheria ya vyama vya ushirika inampa mamlaka ya kutengua uteuzi wa kiongozi yeyote atakayebainika kwenda kinyume hasa kwa kutengeneza makundi na kutoa siri za vikao vya bodi.

Alisema hatua za kisheria zitachukuliwa ikiwamo kuwavua madaraka viongozi watakapobainika kukihujumu chama hicho kwa kujinufaisha wao binafsi na kukwamisha shughuli za ushirika ili kulinda mali na maslahi ya wakulima.

Mwenyekiti wa KACU, Charahani, alisema atahakikisha anasimamia maslahi ya wakuliwa kwa kugawa pembejeo kwa wakati, viuatilifu na kutafuta masoko ili kuhakikisha mkulima ananufaika.

Habari Kubwa