RC ampa OCD siku saba kukomesha mauzo

09Feb 2018
Na Mwandishi Wetu
 MBULU
Nipashe
RC ampa OCD siku saba kukomesha mauzo

MKUU wa Mkoa wa Manyara, Alexander Mnyeti, amesema hataki kusikia gongo ikiendelea kuuzwa wilayani hapa, hususani katika kata ya Dongobesh, na kutoa siku saba kwa Mkuu wa Polisi Wilaya (OCD), Milton Nkyalu, kuhakikisha anamaliza utengenezaji na uuzaji wake.

MKUU wa Mkoa wa Manyara, Alexander Mnyeti.

Mnyeti alitoa agizo hilo juzi wakati akizungumza na watumishi wa Halmashauri ya Wilaya ya Mbulu ambapo alisema ni aibu kuona gongo ikiendelea kuuzwa wakati tayari serikali ilishapiga marufuku pombe hiyo.

"OCD naomba unisikilize na unielewe vizuri sana juu ya hili," alisema Mnyeti. "Mwananchi anakamatwa akiwa anauza gongo anachukuliwa hadi kituoni, anapelekwa mahakamani, kisha unashangaa ile gongo anarudishiwa yule aliyekamatwa".

"Sasa hapa tutakua tunafanya nini kwa wananchi wetu?"

Aidha alimtaka OCD kupanga askari wake kikamilifu ili kuhakikisha wauza gongo wanachukuliwa hatua za kisheria ili kukomesha kabisa biashara hiyo Dongobesh.

"Baadhi ya mambo yanayowaharibia sana jeshi letu la polisi ni pamoja na hili la wananchi kuonekana wakiendelea na kupika gongo, huku bila kujua taifa linaangamia, nyie polisi mpo na mnaangalia tu hiyo hali ikiwa inaendelea, hiyo ndio nguvu kazi ya  taifa letu."

Alisema kwa kuwa ana ziara ya kutembelea kata hiyo ambayo ndio kinara wa uuzaji wa gongo, hatopenda kusikia tena gongo inaendelea kuuzwa katika sehemu yo yote ile.

"Gongo inakamatwa asubuhi... sijui mnazungumza nini huko kituoni, OCD upo, polisi wapo tena wana nguvu kubwa na hii ndio kazi mliyoiomba, unastukia jioni mtuhumiwa anaachiwa," alisema Mnyeti. "Nakupa siku saba kumaliza gongo.

"Ninapokwenda kwenye ziara huko sitaki kusikia gongo, gongo. Inawezekana vijana wako wanakuzunguka, fuatilia hili kikamilifu ili kubaini hili."

Kwa upande wake, OCD Nkyalu alisema amepokea maagizo hayo na atayafanyia kazi haraka iwezekanavyo kama mkuu wa mkoa alivyoelekeza.

 

Habari Kubwa