RC amtumbua mtunza hazina halmashauri

11Jun 2021
Nebart Msokwa
Chunya
Nipashe
RC amtumbua mtunza hazina halmashauri

​​​​​​​MKUU wa Mkoa wa Mbeya, Juma Homera, amemsimamisha kazi Mtunza Hazina wa Halmashauri ya Wilaya ya Chunya, Edward Andendekisye na kuagiza Jeshi la Polisi kuwakamata na kuwaweka ndani watumishi saba wa halmashauri hiyo kutokana na tuhuma za ubadhirifu wa zaidi ya Sh. milioni 400.

​​​​​​​MKUU wa Mkoa wa Mbeya, Juma Homera.

Sambamba na uamuzi huo, pia aliiagiza Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) wilayani hapa kuwahoji watumishi hao.

Alitoa agizo hilo juzi wakati wa kikao maalumu cha Baraza la Madiwani la Halmashauri hiyo lililolenga kujadili ripoti ya Mkaguzi na Mdhibiti Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG).

Aliwataja watumishi wanaotakiwa kukamatwa kuwa ni Edward Mbughi anayedaiwa Sh. milioni 11.6, Lucas Ongala Sh. milioni 16.1, Namwinga Heche Sh. milioni 24, Moses Ludisha Sh. 700,000, Samwel Mwabubili Sh. milioni 14, Gasper Msomba Sh. milioni 11 na Euseius George Sh. milioni nne.

Watumishi wengine wanaotakiwa kuchukuliwa hatua za kiutumishi kuwa ni Ofisa Biashara wa Halmashauri hiyo, Mathias Mbele na Ofisa Mapato, Juma Kapinga.

Homera alichukua hatua hiyo kutokana na halmashauri ya wilaya hiyo kupata hati isiyoridhisha kwenye ripoti ya CAG ya mwaka wa fedha 2019/20.

Mbali na watendaji hao, pia alisema wako watumishi wengine ambao wataendelea kufuatiliwa ambao wamekaa na fedha za halmashauri zaidi ya Sh. milioni 400.9 ambazo ni makusanyo ya fedha za halmashauri.

“Watendaji hawa wanapaswa kusimamishwa kazi na kukaa mahabusu hadi pale watakapolipa fedha wanazodaiwa ambazo pia zimetajwa kuwa chanzo cha halmashauri hii kupata hati isiyoridhisha,” alisema Homera.

Alisema kwa mtendaji atakayeshindwa kulipa fedha anazodaiwa hadi kufikia Juni 25, mwaka huu, atafikishwa mahakamani kujibu tuhuma zinazomkabili. Kwa sasa watakuwa mahabusu chini ya TAKUKURU wakiendelea kuhojiwa.

Awali, Ofisa Mkuu wa Ukaguzi wa Nje (CEA), Michael Magange, alisema Chunya imepata hati hiyo kutokana na sababu mbili ikiwamo tofauti ya ukusanyaji wa mapato katika mfumo.

Magange alisema sababu nyingine ni timu ya ukusanyaji wa mapato, wakiwamo maofisa watendaji kukusanya fedha na kutopeleka katika mfumo wa kibenki zaidi ya Sh. milioni 118 pamoja na halmashauri kushindwa kueleza hatua ilizochukua dhidi ya watumishi wabadhirifu.

Katibu Tawala wa Mkoa wa Mbeya, Dk. Angelina Lutambi, alisema ili mtumishi alipwe stahiki zake ni lazima awajibike katika ukusanyaji wa mapato bila kujali kitengo alichopo.

Dk. Lutambi alisema serikali za mitaa zimepewa mamlaka ya kukusanya mapato ili kuondoa utegemezi kutoka serikali kuu na kutatua changamoto zao wenyewe pamoja na kuwaletea maendeleo wananchi, hivyo suala la ukusanyaji wa mapato ni muhimu.

“Watumishi wote wa serikali tunalipwa mishahara ambayo inatokana na makusanyo kuanzia ngazi ya chini kwa hiyo kila mmoja ambaye amepewa nafasi ya kukusanya mapato lazima awe na weledi,” alisema Dk. Lutambi.

Naye Mbunge wa Jimbo la Lupa, Masache Kasaka, alisema hati isiyoridhisha imetokana na baadhi ya wataalamu kutowajibika katika maeneo yao ikiwamo kuweka makadirio makubwa ambayo yalikuwa hayaendani na uhalisia.

Alisema halmashauri ilikadiria kukusanya zaidi ya Sh. bilioni tano kwa mwaka wa fedha 2018/19 na 2020/21 lakini kiasi kilichopatikana ni Sh. bilioni tatu sawa na asilimia 67.

Habari Kubwa