RC apongeza jiji kwa ubunifu

15Jan 2022
Paul Mabeja
Dodoma
Nipashe
RC apongeza jiji kwa ubunifu

MKUU wa Mkoa wa Dodoma, Anthony Mtaka, amelipongeza Jiji la Dodoma kwa kubuni mradi mkubwa wa soko la machinga, maarufu kama ‘Machinga Open Market’ kwa kutumia mapato yake ya ndani huku akiitaka kampuni iliyopewa zabuni ya kutekeleza mradi huo kukamilisha kwa wakati.

Pongezi hizo alizitoa jana jijini hapa wakati wa ziara ya kukagua eneo hilo na kulipongeza jiji kwa kubuni na kuanza ujenzi wa soko hilo katika eneo la Bahi Road jijini hapa.

Katika ziara hiyo, Mtaka aliongozana na Katibu Tawala wa Mkoa wa Dodoma, Dk. Fatuma Mganga, Mkurugenzi wa Jiji Joseph Mafuru, Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Mkoa na wataalamu kutoka Jiji na Ofisi ya Mkuu wa Mkoa.

“Nikushukuru na kukupongeza Mkurugenzi wa Jiji kwa kuchukua hilo wazo. Wengi wanataka kuona makao makuu yanafananaje. Tunaenda kuwa na soko ambalo nchi hii nzima halmashauri 184 watakuja kujifunza ama kwa kupenda hata kama ni kimoyomoyo kwamba Jiji la Dodoma limekamilisha mradi huu mkubwa,” alisema.

Katika hatua nyingine, Mtaka aliitaka Kampuni ya Mohammed Builders kuhakikisha inakamilisha ujenzi wa mradi huo ifikapo Machi 17, mwaka huu, ili kumpa zawadi Rais Samia Suluhu Hassan ya kutimiza mwaka mmoja tangu awe madarakani.

“Mnajua sababu ya kutaka Machi 17 muwe mmemaliza huu mradi ni kwamba siku hiyo Rais atakuwa anatimiza  mwaka mmoja akiwa madarakani, hivyo nataka tumzawadie zawadi ya hili soko. Naamini litakuwa la kisasa na machinga hawatakuwa wakipata shida,” alisema.

Mtaka pia alisema atawashirikisha wataalamu wote kuhakikisha soko hilo linajengwa kisasa na linakuwa na mahitaji yote ambayo binadamu anatakiwa kupata.

“Ndio maana wataalamu wote wapo hapa. Lengo langu tujenge kitu cha kueleweka hata baada ya miaka kadhaa lakini kubwa nataka halmashauri zote 184 zije zijifunze hapa namna ya kujenga soko bora la wamachinga. Hapa kutakuwa na kila kitu na litakuwa soko la saa 24,” alisema.

Alilitaka Jiji la Dodoma baada ya soko hilo kukamilika kuwaondoa machinga wote waliopo katikati ya mji ili kuliweka jiji katika hali ya usafi.

Katibu Tawala wa Mkoa wa Dodoma, Dk. Mganga alilipongeza Jiji la Dodoma kwa kutenga asilimia 40 ya mapato ya ndani kujenga eneo hilo la wajasiriamali kwa gharama ya zaidi ya Sh. bilioni saba huku akizitaka halmashauri zingine za mkoa huo kuiga mfano kwa jiji hilo.

Kiongozi kutoka Kampuni ya Mohammed Builders, Mohammed Halfaj, alimhakikishia Mkuu wa Mkoa kwamba mradi huo utakamilika muda ambao umepangwa.

Habari Kubwa