RC ataja mwarobaini wa mikopo umiza kwa walimu

24Jul 2021
Paul Mabeja
Dodoma
Nipashe
RC ataja mwarobaini wa mikopo umiza kwa walimu

MKUU wa Mkoa wa Dodoma, Anthony Mtaka, ameitaka Benki ya Biashara ya Mwalimu (MCB) kuja na njia itakayowasaidia walimu kupata mikopo yenye masharti nafuu na kwa haraka ili kuondokana na mikopo umiza.

Mtaka aliyasema hayo jana jijini Dodoma alipokuwa akizindua bidhaa mpya ya Mwalimu na Ujasiriamali iliyoanzishwa na benki hiyo kwa ajili ya kukopesha mashine za uzalishaji mali.

Alisema walimu wamekuwa wakiishi katika mazingira magumu kutokana na aina ya mikopo wanayokopa kutoka katika taasisi ambazo zina masharti magumu na riba kubwa.

Kwa mujibu wa Mtaka, hali hiyo imewafanya walimu kwa muda mrefu kukabiliwa na madeni kutoka taasisi hizo hali ambayo baadhi yao wanalazimika hata kuhama katika vituo vyao vya kazi.

“Lazima ninyi kama Benki ya Mwalimu mwangalie mnakuja kwa utofauti gani na taasisi zingine za kifedha ili kuwakopesha walimu wenye uhitaji kwa ajili ya mambo mbalimbali yanayowakabili bila kuwapatia usumbufu wowote,” alisema Mtaka.

Pia alisema imefikia hatua walimu wanakabidhi kadi zao za benki kwa taasisi za fedha na mishahara inapoingia tu kiasi chote cha fedha kinachukuliwa kwa makato.

Vile vile alisema kuwa benki hiyo inatakiwa kujikita katika kuhakikisha kuwa inakuwa na kitu cha utofauti ambacho kitawavutia walimu na kujiunga nayo.

“Hili jina la mwalimu benki mnaweza kuendelea nalo lakini lazima muone kuwa utendaji wenu uwe kwa ajili ya makundi yote ili kushindana na benki zingine zaidi ya 50 zilizopo nchini,” alisema.

Mtaka pia alisema akiwa Mkuu wa Mkoa wa Simiyu alikuwa anapokea kesi nyingi za walimu kukimbia vituo vyao vya kazi kutokana na madeni hali ambayo inaathiri taaluma katika mkoa husika.

“Kuna vituo vya kazi walimu hawafiki kwa kuhofia kuwa wanaowadai watakuja kudai mikopo yao tena unakuta mwalimu kakopa milioni mbili anakatwa milioni saba,” alisema.

Akizungumzia mpango huo wa mikopo ya mashine za uzalishaji mali, alisema ni ubunifu mzuri ambao kama utasimamiwa vizuri utawawezesha walimu kustaafu wakiwa na tabasamu.

Kadhalika, aliwataka walimu kuchangamkia mkopo huo wa vifaa ambao utawasaidia kujikwamua kiuchumi.

Mtendaji Mkuu wa Benki hiyo, Richard Makungwa, alisema wamejikita katika kutoa huduma za kifedha kwenye ikolojia ya elimu ikiwa pamoja na vyuo vya elimu, walimu, shule, taasisi za elimu, Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia  na TAMISEMI.

“Mwalimu Commercial Bank iliandaa mkakati wa muda mrefu ukiwa na malengo ya kuboresha huduma zenye ubunifu katika kuwafikia wateja wetu,” alisema Makungwa.

Alisema moja ya maeneo yaliyopewa kipaumele ni kuwa na bidhaa zinazolenga moja kwa moja mahitaji ya walimu katika kujiinua kiuchumi na kuleta tija kwenye jamii.