RC awaita wasomi awape ajira

14Oct 2021
Richard Makore
Mwanza
Nipashe
RC awaita wasomi awape ajira

MKUU wa Mkoa wa Mwanza, Robert Gabriel, amewaomba wasomi wote wenye shahada waliopo mkoani humo, kufika ofisini kwake awasaidie kupata mafunzo na mitaji, ili wajiajiri katika sekta mbalimbali, ikiwamo ufugaji wa samaki wa vizimba.

Gabriel alitoa ombi hilo kwa wasomi hao wakati akifungua kikao kazi cha Bodi ya Mikopo ya Elimu ya Juu (HESLB), kilichofanyika jijini hapa jana.

Alisema vijana wote wenye elimu ya juu kupitia mpango maalum atawasaidia kupata mafunzo ya ujasiriamali, mitaji na masoko, kwa ajili ya bidhaa watakazozalisha.

“Ufugaji wa samaki katika Ziwa Victoria hauhitaji kujenga mabwawa, bali wanafugwa kutumia vizimba na kuweka vifaranga vya samaki na mtu anapata mazao bora na mengi," alisema.

Alisema Mkoa wa Mwanza una vijana wengi wasomi, ambao hawana kazi za kuwaingizia kipato na kwamba yeye amejitoa kuwa mwalimu na mtu wa kuwaelekeza namna ya kufanya.

Akizungumza masuala ya mikopo kwa vyuo vikuu hapa nchini, Gabriel alisema, kiwango cha mikopo kimeongezeka kutoka Sh. bilioni 464 kwa mwaka 2020/21 hadi kufikia Sh. bilioni 570 kwa mwaka 2021/22.

Aidha, alisema idadi ya wanafunzi walionufaika na mikopo hiyo kwa mwaka imeongezeka kutoka 149,378 mwaka 2020/2021 hadi kufikia 162,000 mwaka 2021/2022.

Alisema anatamani kuona siku moja Mkoa wa Mwanza unakuwa wa wabunifu katika nyanja mbalimbali, ili kutoa fursa kwa vijana na watu wengine kupata kipato.

Alisifu HESLB kwa kuendelea kutoa huduma bora jambo ambalo limechangia kumaliza migogoro ya wanafunzi katika vyuo vikuu mbalimbali.

Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa HESLB, Abdul-Razaq-Badru alisema lengo la kikao hicho kilichowakutanisha maofisa mikopo kutoka vyuo vikuu vyote hapa nchini ni kuangalia masuala ya utendaji kazi.

Alisema vyuo na taasisi zinazotoa elimu ya juu zipatazo 130, maofisa mikopo wote katika vyuo hivyo wameitwa, ili kujadiliana na HESLB, ili kujua matatizo mbalimbali waliyokutana nayo mwaka ulioisha na kujipanga, kwa ajili ya mwaka ujao wa masomo.

Alisema ili kuwabaini wanafunzi wenye uhitaji wa mikopo ya elimu ya juu, HESLB imeingia makubaliano na Mfuko wa Maendeleo ya Jamii (TASAF), ili wanafunzi wanaotoka familia masikini zinazofadhiliwa na mfuko waweze kupata mikopo.

Kupitia mpango huo wanafunzi ambao kaya zao zinafadhiliwa na TASAF watapata mikopo, wakiwamo yatima, mahitaji maalum na wenye ulemavu.

Alisema kipaumbele ni kwa familia maskini na kwamba kupitia TASAF, watahakikisha wanapata taarifa sahihi za wanafunzi walioomba mikopo ya elimu ya juu.

Kuhusu urejeshwaji wa mikopo kwa wanufaika, Babru alisema kwa mwaka jana walipokea marejesho ya Sh. bilioni 15 na mwaka huu yameongezeka na kufikia Sh. bilioni 18.

Habari Kubwa