RC: Marufuku mawakala kukusanya mapato

17Jun 2021
Nebart Msokwa
Mbarali
Nipashe
RC: Marufuku mawakala kukusanya mapato

​​​​​​​SERIKALI mkoani Mbeya, imepiga marufuku halmashauri zote za mkoa huo kuwatumia mawakala kukusanya mapato na badala yake kukusanya zenyewe kwa kutumia maofisa watendaji wa kata.

​​​​​​​Mkuu wa Mkoa, Juma Homera.

Mkuu wa Mkoa, Juma Homera, alipiga marufuku hiyo juzi wilayani hapa wakati wa kikao maalumu cha Baraza la Madiwani cha kujadili hoja za Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG).

Alisema ukusanyaji wa mapato ya serikali kwa kuwatumia mawakala unachangia kuvuja kwa mapato kwa kuwa baadhi ya mawakala wamekuwa wakikusanya fedha hizo na kukaa nazo bila kuziwasilisha halmashauri.

Mkuu huyo wa mkoa alisema katika Halmashauri ya Wilaya ya Mbarali pekee, kampuni zilizokuwa zinakusanya  mapato zimesababisha upotevu wa zaidi ya Sh. milioni 170 ambazo zilikusanya na kubaki nazo bila kuwasilisha serikalini.

Aliwataka wakurugenzi kusimamia utaratibu huo kwa kuwasimamia maofisa watendaji pamoja na watumishi wengine watakaoaminiwa na kukabidhiwa mashine za kukusanyia mapato hayo.

“Hapa nimeangalia wakala mmoja anadaiwa zaidi ya Sh. milioni 10, mwingine Sh. milioni 12 na mwingine anadaiwa zaidi ya milioni 15 na bado wako wengine. Sasa kuanzia Julai Mosi, mwaka wa fedha utakapokuwa unaanza, ni marufuku mawakala kutumika kwenye ukusanyaji wa mapato,” alisema Homera.

Alisema endapo halmashauri zitakusanya zenyewe, kuna uwezekano zikakusanya zaidi ya ambavyo zimekuwa zikiwatumia mawakala na kwamba katika kila halmashauri alizopita alibaini upotevu wa fedha za serikali.

Katika hatua nyingine, Homera aliwapa wiki moja maofisa watendaji wanane wa kata za Wilaya ya Mbarali kurejesha fedha ambazo walikusanya lakini hawakuziwasilisha serikalini ambazo ziko ni zaidi ya Sh. milioni 40.

Pia alitoa siku 10 kwa kampuni ambazo zlipewa tenda ya kukusanya mapato wilayani hapa lakini hazikuziwasilisha serikalini, kuwasilisha fedha hizo kabla hatua kali za kisheria hazijaanza kuchukuliwa dhidi yao.

“Baada ya muda huo kuisha, naliagiza Jeshi la Polisi kuwakamata na kuwasweka ndani mpaka warejeshe fedha zote walizokusanya na ikiwezekana watafikishwa mahakamani kwa hatua zaidi mpaka fedha hizi zipatikane,” alisema Homera.

Aliwaagiza wakurugenzi kuhakikisha wanasimamia vizuri watendaji ili utaratibu wa kukusanya mapato kuanzia Julai, mwaka huu, wawe wanakaa na fedha za serikali.

Awali akitoa taarifa ya ukusanyaji wa mapato wa Halmashauri ya Wilaya hiyo, Mkuu wa Wilaya ya Mbarali, Reuben Mfune, alisema halmashauri inategemea zaidi mapato yatokanayo na kilimo cha mpunga, mifugo na shughuli ndogo.

Alisema katika Mwaka wa Fedha 2019/20 halmashauri hiyo ilipanga kukusanya Sh. bilioni 4.6 lakini mpaka kufikia Mei ilikuwa imekusanya Sh. bilioni 4.3 na kwamba mpaka kufikia mwishoni mwa mwezi huu itakuwa imefikia asilimia 100 za ukusanyaji.

“Huku tunalima zaidi mpunga, tuna  viwanda 80 ambavyo vinachakata mpunga, lakini tuna maghala mengi ya kuhifadhia mazao ambayo asilimia 90 ni mpunga,” alisema Mfune.

Habari Kubwa