RC Mwanza ataka uaminifu miradi ya serikali

17Jun 2021
Neema Emmanuel
Mwanza
Nipashe
RC Mwanza ataka uaminifu miradi ya serikali

MKUU wa Mkoa wa Mwanza, Mhandisi Robert Gabriel Luhumbi, amesisitiza uaminifu katika utekelezaji wa Miradi ya serikali kwani hakuna mali ya wizi itakayompa mtu sifa bali utendaji kazi, uzalendo, uadilifu, maono, pamoja na kumtanguliza Mungu Ndiyo msingi uliobora katika kuchochea maendeleo.

Mhandisi Luhumbi amesema hayo leo Juni 17, 2021 mara baada ya kujadili utekelezaji wa hoja za Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa hesabu za Serikali kwa hesabu za Halmashauri kwa kipindi cha 2019/2020 wilayani Magu.

Pia aliwaagiza wataalamu wa manunuzi kuhakikisha bidhaa zote zinazonunuliwa ziwe na bei ya soko kwani watapitia miradi yote ili wajiridhishe hiyo ni fedha ya serikali na mali ya umma lazima ilindwe hivyo waongeze bidii kwani wameaminiwa hivyo ni lazima waonyeshe uaminifu .

" Miradi yote inafanyika nchi nzima hivyo mradi wako usije ukawa umetumia fedha nyingi wenzako kidogo hatutakuelewa kabisa ni bora kutumia bei halisi "ameeleza Luhumbi.

Aidha alisisitiza kuweka nguvu kwenye ujenzi  wa zahanati kwani lengo ifikapo 2025 kisiwepo Kijiji ambacho hakitakuwa na zahanati pia kuanzia kesho fedha zote inayoingia asilimia 40 isitumike kwa chanzo chochote bali katika miradi ya maendeleo.

Habari Kubwa