Rico yaja kivingine kusaidia wawekezaji

26Nov 2021
Maulid Mmbaga
DAR ES SALAAM
Nipashe
Rico yaja kivingine kusaidia wawekezaji

MKURUGENZI Mkuu wa kampuni ya Rico Advertising inayojihusisha na utangazaji wa biashara mbalimbali nchini, Renee Docuson amesema wamekuja na ubunifu utakaosaidia wawekezaji wengi nchini kuweza kujitangaza kimataifa.

Akizungumza leo mkoani Dar es Salaam wakati wa uzinduzi wa kampuni hiyo amesema, lengo la kuanzisha Jarida Hilo ni ili kuongeza fursa kwa wafanyabiashara mbalimbali nchini kuweza kujitangaza kupitia kijarida cha Rico ambacho wananchi wa Tanzania na nchi za nje watakipata na kukisoma bure.

Amesema Jarida hilo pia litapatikana kwa njia ya kidigitali na kumuwezesha mtu kulisoma mahali popote alipo, huku akisisitiza kuwa jarida hilo litasaidia kuongeza chachu ya ukuaji wa uchumi nchini kwa kufanikisha biashara nyingi kujulikana ndani na nje ya mipaka ya Tanzania.

“Mfanyabiashara yoyote anakaribishwa kuitangaza biashara yake kupitia Jarida la Rico Advertising, na litakuwa likisambazwa maeneo mbalimbali ikiwemo kwenye Ndege, balozi za Tanzania zilizopo katika mataifa mbalimbali, maeneo ya kitalii, viwandani, Supermarket, pia tunapatikana Mwenge Tower,” amesema Renee.

Pia alibainisha kwamba kwa kuanzia Jarida hilo litasambazwa katika ubalozi wa Tanzania uliopo nchini Uturuki, na alitoa wito kwa wafanyabiashara na wawekezaji wa ndani na nje kuweza kuungana nao katika kutangaza biashara zao ili kuongeza tija na kwa faida ya taifa kwa ujumla.

Habari Kubwa