Risasi kupunguzwa kwenye rangi

14Feb 2016
Efracia Massawe
Nipashe Jumapili
Risasi kupunguzwa kwenye rangi

WADAU wa Programu ya Mazingira ya Umoja wa Mataifa (UNEP) kwa kushirikiana na nchi 15 za Afrika, ikiwamo Tanzania, wamekubaliana kupunguza kiwango cha ukomo cha madini ya risasi katika rangi zinazotumika kwa matumizi mbalimbali katika jamii ikiwamo kupaka majengo.

Waziri wa Nishati na Madini, Prof. Sospeter Muhongo

Maazimio hayo yameisukuma asasi isiyo ya kiserikali ya agenda ya Sinza Dar es Salaam, kulishawishi Shirika la Viwango Tanzania (TBS), kupitisha kiwango cha ukomo wa madini kilichopitishwa na nchi hizo na kukisambaza kwa watengenezaji wa viwanda vya ndani ili kuikinga jamii na athari za madini hayo.

Katibu Mtendaji wa Asasi hiyo, Silvan Mng'anya, alisema wawakilishi wa serikali hizo, kwa kushirikiana na wadau kutoka mashirika ya kimataifa duniani, walikubaliana kushirikiana kusitisha matumizi ya madini ya risasi katika uzalishaji wa rangi ifikapo mwaka 2020.

Alisema maamuzi hayo yameafikiwa na Programu ya Mazingira ya Umoja wa Mataifa (UNEP), mtandao wa asasi zisizo za kiserikali duniani (IPEN), unaohamasisha sera na shughuli zinazosimamia usalama wa kemikali ili kulinda afya ya binadamu na mazingira sasa na vizazi vijavyo.

Kwa mujibu wa Mng’anya, wadau hao, kwa pamoja walikutana mwanzoni mwa Desemba mwaka jana jijini Addis Ababa, ambapo waliangalia upya tafiti za rangi zinazouzwa katika nchi mbalimbali barani Afrika na kubaini kuwa rangi nyingi zina viwango vikubwa vya madini ya risasi.

“Hatua iliyochukuliwa sasa ni kuondoa madini ya risasi katika rangi ili kuwalinda watoto kutokana na athari zitokanazo na madini hayo kwani yanachangia kuathiri afya ya binadamu na mazingira,” alisema Mng’anya.

Habari Kubwa