Sababu serikali mfumo wa kuunda e-RCS

10May 2022
Na Mwandishi Wetu
Dar es Salaam
Nipashe
Sababu serikali mfumo wa kuunda e-RCS

BUNGE limeelezwa kuwa serikali za pande mbili za Muungano ziliunda mfumo wa kielektroniki wa ‘Electronic Revenue Collection System (e-RCS)’ wenye uwezo wa kutambua miamala ya simu inayofanyika.

Naibu Waziri, Wizara ya Fedha na Mipango, Hamad Hassan Chande, alitoa kauli hiyo bungeni jana alipokuwa akijibu swali la Mbunge wa Jang’ombe (CCM), Ali Hassan Omar King.

Katika swali lake, Mbunge huyo alitaka kujua ni lini Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) itasitisha kukusanya na kuzirudisha fedha za Kodi ya Ongezeko la Thamani (VAT)  zilizokwisha kusanywa kutoka kwenye miamala ya mitandao iliyofanywa Zanzibar kwa kuwa kiasi kilichokusanywa ni asilimia 18, lakini fedha zilizowasilishwa Bodi ya Mapato Zanzibar (ZRB) ni asilimia 15 ya kiwango cha fedha ya makato hayo.

Akijibu swali hilo, Chande alisema Sheria za Kodi ya VAT kwa pande zote za Muungano zimeweka msingi wa kutoza na kukusanya VAT pale ambapo huduma inapotolewa.

Alisema huduma ikitolewa Tanzania Bara, TRA inatoza VAT ya asilimia 18 kwa mujibu wa sheria ya VAT inayotumika Tanzania Bara na huduma ikitolewa Zanzibar, ZRB inatoza VAT ya asilimia 15 kwa mujibu wa sheria ya VAT inayotumika Zanzibar.

“Ili kutambua sehemu ambapo huduma imetumika, serikali za pande mbili za Muungano ziliunda mfumo wa kielektroniki ujulikanao kama ‘Electronic Revenue Collection System (e-RCS)’ wenye uwezo wa kutambua miamala yote inavyofanyika na hivyo kusaidia kutunza takwimu sahihi za mauzo yanayotokana na miamala ya mitandao inayofanywa na watumiaji wa kila upande,” alisema.

Alisema mfumo huo unasimamiwa na kamati ya wataalamu wa kodi kutoka TRA na ZRB.

“Mifumo ya kampuni zote za simu hapa nchini imeunganishwa na mfumo wa Serikali wa e-RCS na taarifa za miamala ya mitandao hutolewa kila mwezi ikiainisha bayana huduma zilizotumika Tanzania Bara na zile zilizotumika Zanzibar,” alisema.

Habari Kubwa