Sababu TRA kushindwa kufikia malengo zatajwa

22Oct 2018
Na Mwandishi Wetu
Musoma
Nipashe
Sababu TRA kushindwa kufikia malengo zatajwa

MAMLAKA ya Mapato Tanzania (TRA) Mkoa wa Mara imeshindwa kufikia lengo la makusanyo iliyopangiwa kuanzia Julai hadi Juni mwaka huu.

mkuu wa mkoa wa mara adam malima picha na mtandao

Sababu ya kutofikia lengo hilo metajwa ni kushuka kwa uingizwaji wa vifaa vya uchimbaji madini katika kipindi cha mwaka wa fedha 2017/18 ukilinganisha na mwaka wa fedha 2016/17.

Meneja wa TRA mkoani hapa, Phold Gwamaka, alisema hayo mwishoni mwa wiki alipokuwa anawasilisha taarifa ya makusanyo ya kodi kwa kipindi cha mwaka 2017/18, kwenye kikao cha kawaida cha Kamati ya Ushauri ya Mkoa (RCC).

Alisema katika kipindi hicho idara hiyo ilipangiwa kukusanya lengo la shilingi 91,724.63 na ilifanikiwa kukusanya shilingi 57,120.86 ambayo ni sawa na kiwango cha utendaji kwa asilimia 61.

"Kodi ya forodha Kwenye vifaa vya uchimbaji madini ilikuwa ikichangia asilimia 75 ya makusanyo yote ya forodha mkoa wa Mara, lakini kwa sasa imeshuka hadi kufikia wastani wa asilimia 51,” alisema.

Aidha, alisema changamoto nyingine iliyopelekea TRA mkoani hapa kutofikia lengo la makusanyo hayo ni baadhi ya wafanyabiashara waliokuwa wanapitisha mizigo yao mpaka wa Sirari kwa kipindi cha mwaka wa fedha 2016/17 kuhamia Bandari ya Dar es Salaam kutokana na kuboreka kwa utendaji wa bandari hiyo.

Mwenyeketi wa kikao hicho, Mkuu wa Mkoa huo, Adam Malima, aliitaka Mamlaka hiyo kusogeza huduma zao katika baadhi ya vijiji kama Kirongwe na Shirati wilayani Rorya karibu na mpaka wa Sirari wilaya ya Tarime.

“Ni vyema kutengeneza ushirikiano wenu na taasisi mbalimbali za serikali na binafsi katika kupata taarifa na kuwa karibu na wafanyabiashara ili kutatua changamoto wanazokabiliana nazo katika biashara zao hasa zinazohusiana na utendaji wa mamlaka ya mapato,” alisema.

Habari Kubwa