Sababu uzalishaji korosho kushuka

14Jan 2019
Dege Masoli
Tanga
Nipashe
Sababu uzalishaji korosho kushuka

UZALISHAJI wa zao la korosho mkoani hapa, umeshuka kutoka tani 1,712 zilizovunwa mwaka 2016/17 hadi kufikia tani 1,381 kwa mwaka 2017/018.Mrajisi wa Msaidizi wa Vyama vya Ushirika Mkoa wa Tanga, Jacqline Senzige, alieleza hayo katika kikao cha wadau wa maendeleo  wa zao la
korosho na kutoa maelezo ya hali ya zao hilo kwa kipindi cha miaka mitatu iliyopita.Senzige alieleza pia sababu zilizoshusha uzalishaji wa zao hilo kuwa ni pamoja na mvua za mfululizo zilizonyesha kwa kipindi kirefu na
kusababisha maua kudondoka na kuozesha matunda.

Sababu nyingine kwa mujibu wa Senzige ni mwitikio mdogo wa wakulima kulipokea zao hilo ambalo lilikuwa geni kwao hasa kwa wakulima wa Wilaya ya Handeni na ukosefu wa elimu ya faida ya zao hilo kwa wananchi.Kutokana na changamoto hizo, aliwashauri maofisa ugani waendelee kutoa elimu ya faida za kilimo cha korosho kwa mkulima.Alieleza kuwa  katika halmashauri kumekuwa na uhaba wa vitendea kazi kwa maofisa ugani na ushirika na kuitaka Bodi ya Korosho kwa kushirikiana na halmashauri watatue tatizo hilo kwa kupitia ushuru unaopatikana na mauzo ya zao la korosho.Alizitaka halmashauri zishirikiane na wadau wengine wa maendeleo
kutatua changamoto ya ukosefu wa rasilimali fedha kwa maofisa ugani
kwa ajili ya kuwafikia wakulima kwa wakati, kwa kuwa bodi haiwezi kuhudumia kwa asilimia 100 kutokana na ufinyu wa bajeti uliopo.
Habari Kubwa