Sababu wanachama 83,667 CHF kushindwa kuhuisha uanachama

19Jul 2019
Marco Maduhu
 SHINYANGA
Nipashe
Sababu wanachama 83,667 CHF kushindwa kuhuisha uanachama

WANACHAMA 83,667 wa Mfuko wa Bima ya Afya ya Jamii (CHF) iliyoboreshwa mkoani Shinyanga, wametajwa kushindwa kuhuisha uanachama wao kutokana na sababu mbalimbali ikiwamo hali ya kiuchumi.

Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga, Zainabu Telack.

Kutokana na hali hiyo, wengi walikuwa wakilipiwa na mashirika na baada ya kuachana nao wakakosa fedha.

Hayo yalibainishwa juzi na Mganga Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga, Dk. Rashidi Mfaume, kwenye uzinduzi wa kampeni ya kuhamasisha wananchi kujiunga na CHF iliyoboreshwa, ambayo iliyoandaliwa na wadau wa afya HPSS kwa ufadhili wa Serikali ya Uswisi.

Alisema kumekuwapo na changamoto kwa wanachama wengi wa CHF mkoani humo kushindwa kuhuisha uanachama wao hasa wale ambao walilipiwa fedha na mashirika, na mara baada ya mashirika hayo kuacha kuwalipia nao wakakosa fedha, na kusababisha kutokuwa tena wanachama wa CHF iliyoboreshwa.

“Mwitikio wa wananchi mkoani Shinyanga kujiunga na CHF iliyoboreshwa bado upo chini sana, kutokana na wengi wao kuwa na hali mbaya ya kiuchumi, na kuwa wategemezi wa kulipiwa bima hii na mashirika, na yakisitisha tu huduma na wao ndio unakuwa mwisho wao,” alisema Dk. Mfaume.

“Mkakati uliopo ni maofisa uandikishaji kutembelea kaya zilizoshindwa kuhuisha uanachama wa CHF, na kuwahamasisha kulipa fedha ili waendelee kunufaika na matibabu kwa gharama nafuu, kuhakikisha dawa na vifaa tiba vinakuwapo muda wote kwenye vituo vya kutolea huduma za afya, na kutenga madirisha ya CHF,” aliongeza.

Naye mgeni rasmi kwenye uzinduzi wa kampeni ya CHF iliyoboreshwa, Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga, Zainabu Telack, alitoa wito kwa wananchi na wanachama ambao wameshindwa kuhuisha uanachama wao kuwa kwenye msimu huu wa mavuno ya zao la pamba, pale watakapouza watenge fedha za kulipia CHF.

Alisema kadi ya kujiunga na CHF iliyoboreshwa inakatwa kwa shilingi 30,000, na kuhudumia watu sita kwenye kaya moja ambapo watapata matibabu ndani ya mwaka mzima, kuanzia kwenye zahanati, vituo vya afya hadi kwenye hospitali ya mkoa.

Meneja Mradi wa HPSS mkoani Shinyanga, Dk. Harun Kasale, alisema wamezindua kampeni hiyo baada ya kuona kuwapo na mwitikio mdogo wa wananchi, ambapo kati ya kaya 261,608 za mkoa huo zilizojiunga na CHF ni 25,513 sawa na asilimia 9.8.