Sababu watalii kuongezeka Hifadhi Saanane

25Mar 2020
Daniel Sabuni
Mwanza
Nipashe
Sababu watalii kuongezeka Hifadhi Saanane

HIFADHI ya Taifa ya kisiwa cha Saanane imeongeza idadi ya wataii wa ndani na wa nje katika kipindi cha miaka sita na kufanya jumla yao kufikia 74,890.

Hali hiyo imesababishwa na uhamasishwaji na kutangaza vivutio vilivyomo ndani na nje ya nchi.

Hayo yalielezwa na Kamishna Msaidizi wa Uhifadhi na Mkuu wa Hifadhi hiyo, Eva Mallya, wakati wa programu maalumu ya kutangaza vivutio vilivyomo katika hifadhi hiyo ili kukukuza na kuongeza idadi ya watalii wa ndani.

Mallya alisema kati ya Julai 2013 na Oktoba 2019, hifadhi ilipokea idadi ya watalii wa ndani, wa nje na wa Afrika Mashariki 74,890 ambao ni ongezeko la wageni 5,968 kati ya mwaka wa fedha 2013/2014 na 2018/2019.

Akizungumzia mafanikio ya ongezeko la watalii wa ndani kutembelea hifadhi hiyo, Mallya alisema ni kutokana na juhudi mbalimbali za kutangaza vivutio vilivyomo kwenye shule, taasisi za umma na za watu binafsi pamoja na kufundisha elimu na faida za uhifadhi katika maisha ya binadamu.

“Pamoja na majukumu muhimu na makubwa tunayofanya hapa Saanane, kubwa kabisa ni kuhifadhi mazalia ya samaki, tunafanya doria za mara kwa mara ili majangili wasivue samaki kwa kutumia nyavu ndogo au kwa sumu,” alisema na kuongeza:

“Kwa kufanya hivyo mazalia yako salama na samaki zitaendelea kuzaliana vizazi hadi vizazi, tofauti na hivyo samaki na aina zake zitatoweka.”

Alitaja vivutio vilivyomo Saanane kuwa ni wanyamapori wa asili na wakupandikizwa kama pimbi, fisi maji, paka mwitu, mamba, mijusi na aina mbalimbali za samaki kama sato na sangara, nyoka waina mbali mbali wakiwemo chatu, aina 70 za ndege wahamaji na wakazi.

Habari Kubwa