Sakata nyama kibudu laibukia bungeni

17May 2018
Augusta Njoji
DODOMA
Nipashe
Sakata nyama kibudu laibukia bungeni

SAKATA la jaribio la kuuzwa kwa nyama kibudu kwenye machinjio ya Tegeta jijini Dar es Salaam, limetinga bungeni huku Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Luhaga Mpina, akisema hatua zimechukuliwa ikiwamo kuwaondoa watumishi waliokuwapo kwenye kituo cha ukaguzi mifugo kilichopo Kibaha mkoani Pwani.

Aidha, amesema msako unaendelea kumsaka mmiliki wa machinjio Tegeta ambaye amekimbia.

Kauli ya serikali ilitolewa na Mpina, baada ya sakata hilo kuibuliwa jana bungeni na Mbunge wa Mbinga Mjini (CCM), Sixtus Mapunda, ambaye aliomba mwongozo kwa Mwenyekiti wa Bunge, Mussa Zungu.

Mapunda alisema licha ya serikali kuwa na mkakati wa kuongeza mapato kupitia sekta ya mifugo, kumekuwa na taarifa ya uwapo wa nyama zisizokuwa na bora.

“Mheshimiwa Mwenyekiti kulikuwa na jaribio la kuuzwa nyama kibudu kwenye machinjio ya Tegeta, naomba mwongozo wako katika jambo hili, serikali inatoa kauli gani,” alieleza Mapunda.

Mara baada ya kuomba mwongozo huo, Zungu alimtaka Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera, Bunge, Kazi, Ajira na Wenye Ulemavu, Jenista Mhagama, kujibu mwongozo huo.

Hata hivyo, Mhagama alimwomba Zungu kumpatia nafasi Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Luhaga Mpina kutolea ufafanuzi suala hilo.

Akielezea suala hilo, Mpina alisema bado nyama ya Tanzania ni bora na salama kwa walaji licha ya uvumi kuhusu uuzwaji wa nyama kibudu na zisizokuwa bora, vyombo vya udhibiti vinafanyakazi kwa umakini kuzuia nyama za aina hiyo kutoingia sokoni.

Aliliambia Bunge kuwa katika tukio la Tegeta lori la mifugo ambalo lilikuwa likitokea Morogoro kuelekea kwenye machinjio ya mifugo Tegeta, lilikutwa na ng’ombe 54 kati yao 42 walikuwa wazima, 12 ilikuwa mizoga ambayo minne ilikwisha chunwa ngozi na miwili ilikwishakatwa vipande.

Alieleza kuwa tukio hilo lilisababisha taharuki kutoka kwa wananchi hususan wanaoishi karibu na machinjio hayo wakihofia usafi na usalama wa maisha yao.

Mpina alisema kwa mujibu wa Sheria ya Magonjwa ya Wanyama ya 2013 na kwa mujibu wa Sheria ya Nyama namba 10 ya mwaka 2016 na kwa Mujibu wa Sheria ya Chakula, Vipodozi na Dawa, tukio hilo lilikuwa kinyume cha sheria.

“Baada ya kubaini tukio hilo ni kinyume cha sheria wizara kwa kushirikiana na Halmashauri ya Kinondoni, ilichukua maamuzi ya kufunga machinjio ya Tegeta, kwa muda usiojulikana.Mpina alibainisha kuwa hatua nyingine iliyochukuliwa ni kuteketeza mizoga hiyo kisha kuifukia na kuondolewa watumishi waliokuwapo kwenye kituo cha ukaguzi mifugo kilichopo Kibaha mkoani Pwani,” alisema.

Mbali na hilo, alisema mmiliki wa lori hilo amekwisha kamatwa huku msako ukiendelea kumsaka mmiliki wa machinjio hayo ambaye amekimbia.

Alisema vyombo vya ukaguzi, vina usimamizi madhubuti katika mabucha na machinjio kuwahakikishia walaji, hivyo wananchi wasiwe na shaka na mtu yeyote kwani nyama za Tanzania ni bora zinazotokana na malisho bora.

“Tunawahakikishia usalama, kwa tukio hilo la jaribio ndio maana wahusika walikamatwa,” alibainisha.

Tukio hilo lililotokea Jumapili, lilizua taharuki ambapo picha za mizoga hiyo ya ng’ombe zilisambazwa kwenye mitandao mbalimbali ya kijamii.

Habari Kubwa