Samia aonya benki mitandao uhalifu

15Jun 2019
Paul Mabeja
DODOMA
Nipashe
Samia aonya benki mitandao uhalifu

MAKAMU wa Rais, Samia Suluhu Hassan, imezitaka benki kuepuka kujiingiza katika kashfa na mitandao ya kutakatisha fedha kinyume na matakwa ya Sheria ya Benki na Taasisi za Kifedha na sheria zingine za nchi.

Samia aliyasema hayo jana wakati akifungua tawi la Benki ya Biashara ya Mkombozi jijini Dodoma.

Alisema benki zinapaswa kuwa makini katika kuhakikisha kuwa katika utendaji wa kazi wa kila siku kutojiingiza katika kashfa yoyote ya utakatishaji wa fedha.

Kwa mujibu wa Samia, vitendo hivyo vya utakatishaji fedha vitachangia katika kuharibu sifa ya benki hali ambayo wateja watakosa imani nayo.

Aidha, aliwataka Watanzania kujijengea tabia ya kutumia huduma za kibenki na kuacha kulala na fedha chini ya mito ya vitanda.

"Watanzania lazima tubadilile, tuache kuhifadhi fedha zetu ndani ya nyumba. Kuna  watu hadi leo hii wanalala na fedha chini ya mito ya vitanda vyao wakiamini kuwa ziko salama, lakini si kweli. Mnachotakiwa  kufanya ni kutumia huduma za kibenki kwani hata leo hii benki ikifilisika hela zenu mnazipata kwa mujibu wa sheria," alisema Samia.

Pia aliitaka benki ya Mkombozi na zingine kuhakikisha zinaangalia namna ya kuweka riba nafuu, ili kuwezesha vikundi na wafanyabiashara wadogo kukopa na kurejesha kwa urahisi.

"Suala la riba kwa wajasiriamali wadogo pamoja na wafanyabiashara wadogo bado ni changamoto sana. Benki nyingi bado zinariba za juu sana, hivyo basi niwaombe ninyi mwangalie namna ya kupunguza riba hiyo, lakini niwapongeze kwa kuwezesha vikundi kukopa kwa kujidhamini,” alisema.

Makamu huyo wa Rais pia alizitaka benki na taasisi za kifedha nchini kubadili mfumo wa ujazaji fomu za kufungua akaunti kwa wateja ili kutumia lugha ya Kiswahili.

Alifafanua kuwa benki nyingi zimekuwa zikihamasisha wananchi kufungua akaunti kwa lugha ya Kiswahili na wakati mwingine hata kwa lugha mama ili kuwapata wateja, lakini jambo la kushangaza ni ujazaji wa fomu kutumia lugha ya Kiingereza.

Naye Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa Mkombozi, Thomas Enock, alisema kuwa benki hiyo ilianzishwa miaka 10 iliyopota ikiwa na mtaji wa Sh. bilioni sita, lakini sasa umefikia Sh. bilioni 20.