Samia kuboresha vitambulisho vyao

26Jan 2022
Romana Mallya
Dar es Salaam
Nipashe
Samia kuboresha vitambulisho vyao

RAIS Samia Suluhu Hassan, ameahidi kuviboresha vitambulisho vya machinga kwa kuvitengeneza vipya ambavyo vikiingizwa kwenye mashine vitatoa taarifa zao na kuwawezesha kupata huduma sehemu yoyote.

Alitoa ahadi hiyo jana Ikulu jijini Dar es Salaam wakati akizungumza na viongozi wa wafanyabiashara wadogo (machinga).

Rais Samia alisema vitambulisho hivyo vitawawezesha kwenda sehemu yoyote, vitawafaa kufanya navyo kazi au kupata huduma.

“Kitambulisho ambacho kitakuonyesha wewe ni nani, sasa hili tunasubiri tumalize sensa ya watu na makazi na mbali ya sensa tunasubiri maeneo ambayo tumeamua kuyajenga kwa sasa, kama Kariakoo, Jangwani na Karume, tutakapotoa kitambulisho tunamjua Lusinde kituo chake cha kazi ni Jangwani, ana miaka hii, biashara yake ni hii, ana watoto hawa,” alisema Samia.

Alisema hawataharakisha kuvitengeneza kwa sababu vitakuwa vya gharama, hivyo amewataka wamachinga kuwa na subira ili vikitengenezwa viwe vyao daima.

Pia aliwaomba baada ya maboresho hayo kundi hilo lilipe kodi kwa kadri ya biashara zao ili serikali iendelee kuboresha miundombinu yao na kutoa huduma.

Kadhalika, aliwataka viongozi wa machinga kulitazama suala la wenye maduka kuwapa machinga bidhaa zao ili kuwauzia kwa sababu mwenye kodi akipita dukani, mashine za EFD’s hazionyeshi mauzo kwao.

Akizungumzia mchakato wa kuwapanga kwa kuwaondoa maeneo yasiyo rasmi, Rais Samia alisema kuna watu walisubiri vurugu zitokee, nchi iharibike lakini machinga wa Dar es Salaam walikuwa waungwana na wazalendo.

Pia alitoa pole kwa machinga baada ya kutokea kwa tukio la moto katika masoko ya Kariakoo na Karume.

Alisema Soko la Kariakoo lilipoungua sababu ilitajwa ni umeme na Karume taarifa za awali ni mshumaa.

“Lakini, moto unapoendelea hata magari ya kuzima moto yanapofika yanakosa sehemu ya kupita, mtakaporudi Karume mjipange ili itakapotokea hitilafu magari yaweze kupita na kuuzima,” alisema Samia.

Rais Samia alisema serikali inawatambua machinga katika mipango yote inayopanga ukiwamo mpango wa miaka mitano uliomalizika, wa pili na wa tatu ambao chini ya Hayati Rais John Magufuli aliwatambua kwa kutengeneza vitambulisho.

Aidha, Rais Samia aliwataka wakurugenzi, wakuu wa mikoa na wilaya kusimamia maslahi ya machinga na kuendelea na mchakato na kuyafanyia kazi matatizo yao.

Habari Kubwa