Sekta ya utalii ina nafasi ya kukuza uchumi

20Mar 2019
Na Mwandishi Wetu
Zanzibar
Nipashe
Sekta ya utalii ina nafasi ya kukuza uchumi

AFRIKA Kusini na Zanzibar zina nafasi kubwa ya kuimarisha ushirikiano katika kuitumia sekta ya utalii kwa ajili ya kukuza uchumi wa nchi hizo.

Hayo yameelezwa na Waziri wa Habari, Utalii na Mambo ya Kale, Mahmoud Thabit Kombo, wakati akizungumza na Balozi wa Afrika Kusini nchini Tanzania, Thami Mseleku, aliyemtembelea ofisini kwake.

Waziri Kombo alisema hilo litawezekana kwa kuanzisha jukwaa la pamoja litakalojikita katika kuinua sekta hiyo.

Alilitaka jukwaa hilo lijumuishe wizara mbalimbali za serikali na taasisi binafsi zinazojishughulisha na utalii zikiwamo Jumuiya ya Wafanyabiashara, Wenye Viwanda na Wakulima Zanzibar, Jumuiya ya Wawekezaji wa Sekta ya Utalii Zanzibar (ZATI).

Alimshauri balozi huyo kuangalia uwezekano wa kulitaka Shirika la Ndege la Afrika Kusini (Mango), kuongeza idadi ya safari zake za moja kwa moja Zanzibar ili kuleta wageni wengi zaidi, na hivyo kutunisha mfuko wa fedha za kigeni.

"Kwa sasa ndege ya Afrika Kusini inatua takriban kila siku hapa Zanzibar, mwaka 2018 tulipokea wageni 22,903 kutoka nchi hiyo na mwaka huu tunatumai itapanda zaidi," alisema.

Kuhusu umuhimu wa kuzitunza historia za Afrika Kusini, Zanzibar na Tanzania kwa jumla ili zifahamike na wageni na kizazi cha sasa, Waziri Kombo ameipongeza nchi hiyo, kwa uamuzi wake wa kuanzisha makumbusho jijini Dar es Salaam, yatakayokuwa na historia ya ukombozi wa nchi hiyo.

Kwa upande wake, Balozi Thami Mseleku, alisema hakuna namna yoyote inayoweza kuitenganisha nchi yake na Tanzania, ambayo chini ya Hayati Mwalimu Julius Nyerere, ilitoa mchango mkubwa katika ukombozi wa Afrika Kusini na nchi nyingine za Afrika.

Alisema haitoshi Tanzania na Afrika Kusini kujiona ni marafiki, kwa kuwa kimsingi mataifa hayo ni sawa na ndugu wa mama na baba mmoja kutokana na mambo mengi yanayowaunganisha.

Alieleza kuwa, atatumia nafasi ya uwakilishi wa nchi yake kuwashajiisha wawekezaji zaidi kuwekeza Zanzibar na Tanzania kwa jumla katika miradi ya kiuchumi ikiwamo utalii.

"Naelewa kuwa Zanzibar kuna hoteli sita za Waafrika Kusini, huu ni mwanzo mzuri na katika ziara yangu hii natarajia kukutana nao pamoja na watendaji wa Kamisheni ya Utalii Zanzibar ili tuzungumze namna ya kuimarisha zaidi sekta hii," alisema Balozi Mseleku.

Habari Kubwa