Sekta ya viwanda kupunguza tatizo la ajira

12Jan 2018
Rahma Suleiman
Nipashe
Sekta ya viwanda kupunguza tatizo la ajira

 WAZIRI Mkuu Kasim Majaliwa, amesema kufanikiwa katika uzalishaji wa sekta ya viwanda na kuongeza uzalishaji wa bidhaa mbalimbali kutapunguza kiwango kikubwa cha ukosefu wa ajira nchini.

 WAZIRI Mkuu Kasim Majaliwa.

Akifungua tamasha la nne la biashara Zanzibar, alisema  ndio maana Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imeamua kupunguza tatizo la ajira kwa kukaribisha wawekezaji nchini katika sekta ya viwanda.

Alisema, biashara sasa ni mkakati katika kutafuta soko hivyo ni busara kuangalia nchi zenye soko kubwa la biashara ili kujua bidhaa zinazohitajika na zenye ubora.

Alisema tamasha la biashara linaweza kuwa nyenzo muhimu katika kuanzisha uhusiano mzuri ili kukuza biashara kati ya mteja na mfanyabiashara.

”Tamasha hili ni muhimu na fursa pekee kwa taasisi za serikali na binafsi,” alisema Majaliwa, katika tamasha hilo ikiwa ni shamrashara za miaka 54 ya Mapinduzi ya Zanzibar.

Aliitaka Wizara ya Biashara, Viwanda na Masoko Zanzibar, kulitupia tena jicho tamasha hilo na kuwa chachu ya kukuza utalii kama ilivyo kwa nchi zingine zinavyotangaza soko na kuvutia utalii kupitia matamasha kama hayo na kutoa mfano wa Dubai na Malaysia.

Aidha, alisema kuimarika kwa tamasha hilo ni chachu ya biashara na kuirejesha Zanzibar katika hadhi yake ya kuwa ni kitovu kikuu cha biashara katika Afrika Mashariki.

Alisema Serikali ya Zanzibar chini ya Dk. Ali Mohamed Shein, imeweka wazi suala la uwekezaji katika biashara na viwanda kwa kuongeza fursa za uwekezaji na vivutio vyote vya uwekezaji katika sekta mbalimbali ikiwamo utalii, biashara, viwanda, kilimo, uvuvi wa bahari kuu, ujenzi wa nyumba na sekta iliyoibuka ya gesi na mafuta.

Alisema sekta zote hizo zina fursa ya kuleta maonyesho yao ili wananchi waweze kujionea, hivyo matumaini yake ni wafanyabiashara kuichangamkia fursa hiyo ya uwekezaji.

“Wafanyabiashara ni lazima kuchangamkia fursa ili tamasha lijalo litawaliwe na bidhaa nyingi zinazozalishwa nchi kupitia sekta ya kilimo na uvuvi,” alisema.

Alisema tamasha hilo litakuza uhusiano wa kibiashara kutoka Tanzania bara na Afrika Mashariki na kusisitiza tamasha hilo lipewe nguvu, kuliendeleza na kulipa uwezo.

Aidha, alisema matamasha hayo yana faida nyingi ikiwamo kutoa fursa kwa wafanyabiashara kukutana na wateja wao na kupata mrejesho jinsi bidhaa yake inavyokubalika katika soko na kukuza uchumi wan chi.

Waziri wa Biashara, Viwanda na Masoko, Balozi Amina Salum Ali, alisema  Serikali ya Zanzibar imepiga hatua kubwa katika kuweka mazingira bora ya biashara kwa kupunguza urasimu wa kufanya biashara, kuweka sheria ya ushindani halali na mamlaka ya kushawishi viwanda vidogo na vya kati.

Naye Katibu Mkuu Wizara ya Biashara Zanzibar, Dk. Juma Ali Juma, alisema kuwa tamasha hilo linawashiriki 230 na limepanua wigo kwa kuwa na washiriki kutoka Zanzibar, Tanzania bara, Kenya,Uganda, Burundi, Misri na Uturuki.

 

Habari Kubwa