Serikali kufuta mikopo

30Apr 2019
Augusta Njoji
DODOMA
Nipashe
Serikali kufuta mikopo

SERIKALI imesema inakusudia kuyafuta malimbikizo ya fedha za mikopo ya vijana na wanawake ya miaka ya nyuma iliyotakiwa kutolewa kabla ya mwaka 2016 lakini haikutolewa na halmashauri kwa walengwa.

Hatua hiyo inatokana na maelekezo yaliyotolewa na Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali za Mitaa (LAAC) kufuatia malimbikizo hayo kusababisha uwapo wa hoja za ukaguzi kutoka kwa Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG).

Kusudio hilo lilitangazwa jana bungeni na Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa(Tamisemi), Mwita Waitara, alipojibu swali la Mbunge wa Lupembe, Joram Hongoli (CCM).

Mbunge huyo alisema madeni ya halmahauri hususani mikopo ya vijana na wanawake ya miaka ya nyuma kabla ya 2016 yamekuwa hayalipiki kutokana na halmashauri nyingi kutokuwa na mapato ya kutosha kuendesha halmashauri hizo hasa miradi ya maendeleo.

"Je, ni kwanini madeni hayo yasifutwe ili kuondoa hoja za ukaguzi kwenye halmashauri hizo? mbunge alihoji.

Akijibu swali hilo, Waitara alisema kwa sasa, kazi ya uhakiki wa takwimu kubaini kiasi ambacho kimelimbikizwa katika halmashauri zote nchini inaendelea na mara tu itakapokamilika taratibu za kufuta malimbikizo hayo zitafanyika.

Alisema kwa sasa, Ofisi ya Rais, Tamisemi inazisimamia kwa karibu halmashauri ili kuhakikisha zinatoa fedha hizo kwa mujibu wa sheria ambayo inasimamia utoaji mikopo hiyo.

Awali, Waitara alieleza kuwa mamlaka za serikali za mitaa zimekuwa zikitoa fedha za mikopo kwa ajili ya vikundi vya wanawake, vijana na watu wenye ulemavu inayotokana na asilimia 10 ya mapato ya ndani ya halmashauri kwa kuzingatia maelekezo ya serikali.

Alisema katika kipindi chote cha utekelezaji hakukuwa na sheria kwa ajili ya kusimamia utengeji na utoaji mikopo hiyo na kusababisha kuwapo kwa changamoto mbalimbali ikiwamo malimbikizo ya fedha ambazo hazikutolewa kwa walengwa katika kipindi husika na kusababisha hoja za ukaguzi kutoka kwa CAG.

Habari Kubwa