Serikali kukusanya Sh. trilioni 1.025 mwezi huu

21Apr 2016
Gwamaka Alipipi
Dar es Salaam
Nipashe
Serikali kukusanya Sh. trilioni 1.025 mwezi huu

KATIKA jitihada za kuongeza makusanyo ya kodi, serikali imejiwekea lengo la kukusanya Sh. trilioni 1.025 kwa mwezi huu.

Richard Kayombo.

Akizungumza na Nipashe, Mkurugenzi wa Huduma na Elimu kwa Mlipa Kodi wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), Richard Kayombo, alisema kwa Aprili, wamejiwekea malengo ya kukusanya kiasi hicho cha fedha.

“Kwa Aprili, lengo tulilojiwekea la kukusanya ni Sh. 1,025,585,000,000, ila tunaweza tukavunga lengo hilo,” alisema Kayombo.

Tangu serikali ya Rais Dk. John Magufuli, kuingia madarakani Novemba 5, mwaka jana, ukusanyaji wa kodi umekuwa ukiongezeka na kushuka.

Mathalan, Novemba, mwaka jana, mapato yalipanda kutoka wastani wa Sh. bilioni 800 na Sh. bilioni 900 kwa mwezi mpaka kufikia Sh. trilioni 1.3.

Aidha, Desemba, mwaka jana, ukusanyaji uliongezeka hadi kufikia Sh. trilioni 1.4 na Januari mwaka huu, yalikuwa Sh. trilioni 1.06, huku Februari makusanyo yakifikia Sh. trilioni 1.04 na Machi, mwaka huu TRA ilikusanya Sh. trilioni 1.316 sawa na asilimia 101.0 ya lengo la kukusanya Sh. trilioni 1.302.

Itakumbukwa kuwa wakati akilihutubia Bunge mjini Dododoma Novemba 20, mwaka jana, Rais Dk. Magufuli alisema kwa zaidi ya miaka mitatu sasa, ukusanyaji wa mapato umekuwa chini ya makadirio kwa sababu mbalimbali.

Alisema Serikali ya Awamu ya Tano itaongeza nguvu katika upanuzi wa wigo wa kodi na kuongeza ufanisi katika ukusanyaji wa mapato.

“Tutahakikisha kwamba kila mtu anayestahili kulipa kodi analipa kodi stahiki. Hatutasita kumchukulia hatua mtu yeyote atakayekwepa kulipa kodi. Tunawaomba wananchi mhakikishe mnapewa risiti kila mnaponunua bidhaa au huduma. Kodi ni kitu muhimu, lazima kila mtu anayestahili kulipa kodi alipe," alieleza Rais Magufuli katika hotuba hiyo.

Rais Magufuli pia alieleza kuwa serikali yake itahakikisha kwamba kila senti inayoongezeka katika mapato yke, inaelekezwa katika kutoa huduma bora zaidi kwa wananchi kwa kuziba mianya ya upotevu wa fedha za serikali ambayo inaipunguzia serikali uwezo wake wa kuwahudumia wananchi.

Habari Kubwa