Serikali kutowapangia bei wakulima wa Tumbaku

06Feb 2016
Beatrice Shayo
Nipashe
Serikali kutowapangia bei wakulima wa Tumbaku

Naibu Waziri wa Kilimo Mifugo na Uvuvi, William Ole Nasha amesema bei ya tumbaku hupangwa na wadau wenyewe kadri wanavyoona inawalipa na si serikali.

Ole Nasha aliyasema hayo jana bungeni wakati akijibu swali la nyongeza la mbunge wa Urambo, Margaret Sitta (CCM).
Mbunge huyo alitaka kujua kama serikali ina mpango wa kupanga bei ya tumbaku ili kuondokana na bei ndogo ambayo wakulima hupata licha ya kuwa wanatumia nguvu nyingi na muda mwingi katika kulimo hicho.
Katika swali la nyongeza, Sitta alisema wakulima wa tumbaku hutumia muda mwingi na fedha nyingi lakini wanapofikia hatua ya kuuza tumbaku huuzwa kwa bei ndogo jambo ambalo huwakatisha tamaa wakulima.
Kutokana na hali hiyo, Sitta alitaka kujua kama serikali ina mpango wowote wa kupanga bei ya tumbaku ili wakulima waweze kupata faida na kufurahia kilimo cha zao hilo "ambalo huliingizia taifa pato kubwa."
Awali katika swali la msingi la mbunge huyo alitaka kujua ni kwanini hasara inayotokana na matatizo ya wakulima kupata pembejeo kwa bei kubwa na wakati huo huo inapotokea kushuka kwa bei ya tumbaku, mzigo hubebwa na wakulima.
Pia alitaka kujua serikali imejipanga vipi kuondoa matatizo yanayowakabili wakulima wa tumbaku ili wanufaike na kilimo na hatimaye wajikwamue kiuchumi.
“Je, ni kwanini hasara inayotokana na matatizo hayo ibebwe na wakulima pekee. Ni kwa nini serikali isihusike katika hasara hiyo,” alihoji Sitta.
Akijibu maswali hayo, Ole Nasha alisema serikali haina mpango wowote wa kupanga bei ya zao la tumbaku badala yake wadau na wakulima ndio wenye jukumu la kupanga bei ya zao hilo kadri watakavyoona inawapatia faida.
Hata hivyo alisema serikali inaendelea kuchukua hatua dhidi ya changamoto zinazowakabili wakulima wa zao la tumbaku.
Alisema hatua hizo ni pamoja na kuboresha mfumo wa upangaji wa bei ya tumbaku ambapo wakulima hupendekeza bei yenye tija kwao na kuiwasilisha kwa wanunuzi kupitia katika vikao vya halmashauri ya tumbaku.

Habari Kubwa