Serikali kuwajengea uwezo wakulima wa kahawa Songea

08Dec 2023
Gideon Mwakanosya
SONGEA
Nipashe
Serikali kuwajengea uwezo wakulima wa kahawa Songea

Naibu Waziri wa Kilimo, David Silinde amesema serikali kupitia wizara hiyo imejipanga kuongeza uzalishaji wa zao la kahawa kwakuwa zao hilo ni la kimkakati linaloliingizia Taifa fedha nyingi za kigeni.

Naibu Waziri wa kilimo David Silinde akipata maelezo toka kwa mmoja wa wakulima wa zao la Kahawa wa Kata ya Wino katika Halmashauri ya Wilaya ya Madaba ambako Taasisi ya Utafiti ya zao la Kahawa( TaCRI) kituo cha UGANO Wilayani Mbinga kimeweza kutoa mafunzo ya elimu ya kilimo cha zao la Kahawa ambao wameweza kuandaa vitalu vya miche ya kahawa aina ya Kompakti ambayo inagawiwa bure kwa wakulima.

Silinde, amehimiza wakulima wa zao hilo wilayani Songea kuona umuhimu wa kujikita katika kuhakikisha wanalima kahawa badala ya kutegemea mazao machache likiwemo zao la mahindi.

Silinde ambaye ni Mbunge wa Tunduma mkoani Songwe aliyasema hayo jana wakati akiwahutubia wadau wa zao la kahawa mkoani Ruvuma kwenye ukimbi wa mikutano wa Halmashauri ya Manispaa Songea.

Alisema kuwa lengo kubwa la serikali ni kuhakikisha kuwa wakulima wa zao la Kahawa hasa wa Wilaya ya Songea ambako wanamaeneo mazuri yanayoweza kulimwa na zao hilo wakilima watapata ushirikiano wa kutosha ili kuweza kuongeza uzalishaji wa zao la Kahawa katika maeneo hayo pia pamoja wakulima wa Kahawa maeneo mengine na si vinginevyo.

Alifafanua kuwa selikali kupitia wizara yake inashauri mkulima wa zao hilo kulima zaidi ya mara moja tofauti na ilivyo zoeleka ya kulima mara moja kipindi cha msimu wa mvua na amefafanua kuwa katika kuhakikisha kuwa sereikali imedhamiria kuboresha kilimo kila Wilaya hapa nchini mpango upo mzuri wa kuhakikisha kuwa kunakuwa na bwawa ambalo litaweza kusaidia zaidi kilimo cha umwagiliaji na amewahimiza wakulima wa zao hilo waone umuhimu wa kupanda miche bora ya kisasa ya zao la kahawa iliyo fanyiwa utafiti wa kutosha na Taasisi ya Utafiti wa Zao la Kahawa Tanzania( TaCRI).

Alisema kuwa TaCRI kupitia kituo cha utafiti cha UGANO kilichopo Wilayani Mbinga kinafanya kazi nzuri na ndicho kinachowawezesha wakulima wa zao la Kahawa Mkoani humo kuwapa mafunzo ya kilimo bora cha zao la Kahawa pia na kuwapatia bure miche ya Kahawa hasa wakulima wa Halmashauri za Wilaya ya Songea,Madaba pamoja na Manispaa ya Songea.

Ditriki Henjewele mkazi wa Kijiji cha Kilagano Wilayani Songea alisema kuwa serikali kupitia Wizaera ya Kilimo imeweza kuwasaidia wakulima wengi wa zao la Kahawa kwani awali walikuwa na mawazo ya kuwa maeneo ya Songea hayafai kwa kilimo cha zao la Kahawa jambo ambalo walidai kuwa si kweli kwani katika kijiji cha Kilagano kwa wale wananchi waliojitokeza kujikita katika kilimo cha zao la kahawa wamenufaika na mambo mengi ikiwemo kusomesha watoto.

Eliasi Mwale mkazi wa kijiji cha Maposeni Wilayani Songea aliipongeza serikali kupitia kituo cha utafiti wa zao la Kahawa (TaCRI) cha UGANO kwa kuwajengea uwezo wakulima wa maeneo hayo kulima zao la Kahawa ambapo kwa muda mrefu walikuwa wakilima zao la mahindi tu lakini kwa sasa hivi wataalamu kutoka UGANO wamekuwa wakipita kwenye vijiji vyao  kutoa elimu ya kilimo bora cha zao la Kahawa ambapo wananchi wengi wameona umuhimu na wamehamasika kulima zao hilo ambalo limekuwa likileta faida kubwa sana baada ya mavuno tofauti na mazao mengine.

Mapema Mkuu wa Wilaya ya Songea  Wilman Ndile akimkaribisha mgeni rasmi Naibu Waziri Ndile kwenye kikao hicho cha wadau wa Kahawa alisema kuwa zao la Kahawa ni la kimkakati na kwa Wilaya ya Songea Kahawa inalimwa katika Halmashauri zote tatu na bei ya zao hilo imekuwa ikipanda kila mwaka na ni zao linalo kopesheka kwenye taasisi za fedha kiurahisi tofauti na mazao mengine hivyo ni vyema wakulima wakaona umuhimu wa kuongeza bidii ya kulima zao hilo na si vinginevyo.