Serikali yaahidi bei elekezi ya pamba, 1,000/-

22Jun 2016
Rose Joseph
Mwanza
Nipashe
Serikali yaahidi bei elekezi ya pamba, 1,000/-

CHAMA kinachotetea wakulima wa zao la pamba nchini (Tacoga), kimeibuka kidedea baada ya kutaka bei ya zao hilo kupanda bei.

Hivi karibuni kuliibuka mvutano mkubwa kati ya wafanyabiashara na wakulima wa zao hilo kuhusu bei ya zao hilo huku wakulima wakitaka kuuza kio moja kwa Sh. 1,145, wakati wanunuzi wakitaka kwa 643, hali iliyofanya wakulima kupinga na kutishia kutolima zao hilo.

Hata hivyo, juhudi za wakulima kufikisha suala lao Wizara ya Kilimo, Uvuvi na Mifugo kwa Waziri Dk. Charles Tizeba, zilifanikiwa kutatua changamoto hiyo.

Mwenyekiti wa Tacoga, Godfrey Masaga, aliyeongozana na viongozi, walikutana na Dk. Tizeba na Waziri Mkuu Kassim Majaliwa, mjini Dodoma ili kumaliza mvutano huo.

Masaga alisema, Waziri Mkuu Majaliwa alikiri Serikali kulisahau zao hilo na kwamba kilimo hicho kwa muda mrefu kimebaki mikononi mwa wananchi bila kuwapo kwa mkono wa serikali, hivyo kuwaahidi wakulima kushirikiana nao.

Aidha, alisema Waziri Mkuu aliahidi bei elekezi ya msimu huu, iwe Sh. 1,000 kwa kilo na mfanyabiashara asiyetaka kununua kwa bei hiyo, aachane na boashara hiyo.

“Tunamshukuru sana Waziri Mkuu kwa maamuzi aliyoyatoa kwani awamu zote za uongozi zilizopita hazikuwahi kutoa maamuzi magumu kama hayo,” alisema Masaga.

Habari Kubwa