Serikali yaahidi kushirikiana na vyuo binafsi

25Nov 2018
Na Mwandishi Wetu
Dodoma
Nipashe Jumapili
Serikali yaahidi kushirikiana na vyuo binafsi

WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amesema serikali itaendelea kushirikiana na vyuo vikuu vyote nchini katika kutoa elimu ya juu yenye ubora na viwango vinavyotakiwa kwa lengo la kukidhi matakwa na ushindani kwenye soko la kitaifa na kimataifa.

WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa, picha na mtandao

Majaliwa aliyasema hayo juzi kwenye mahafali ya tisa ya Chuo Kikuu cha Mtakatifu Yohana cha Tanzania Kampasi ya Chifu Mazengo, Dodoma, yaliyofanyika kwenye ukumbi wa CCM.

Alisema suala hilo ni muhimu likapewa uzito unaostahili kwa kuwa wahitimu hao wakitoka vyuoni wanakwenda kutoa huduma katika jamii ya Watanzania na kimataifa, hivyo ni muhimu elimu inayotolewa ikazingatia ubora na viwango vinavyostahili.

Majaliwa alisema serikali inatambua na kuthamini mchango wa sekta binafsi hususan wa vyuo vikuu binafsi kama Chuo Kikuu cha Mtakatifu Yohana cha Tanzania, katika maendeleo ya elimu ya juu.

"Serikali inatambua mchango wa vyuo hivyo katika kupanua fursa kwa Watanzania wengi kupata elimu ya juu. Hadi sasa udahili wa wanafunzi wa elimu ya juu kwenye vyuo vikuu binafsi nchini ni takriban asilimia 25 ya wanafunzi wote," alisema.

Alisema serikali inatambua mchango wa chuo hicho katika kutayarisha watalaamu wa fani mbalimbali na kwamba tangu kuanzishwa kwake mwaka 2007, kimetoa zaidi ya wahitimu 10,000.

Miongoni mwa wahitimu hao, kwa mujibu wa Majaliwa, wamo wafamasia, wauguzi, walimu wa sayansi, walimu wa sanaa, wataalamu wa maabara na wasimamizi na waendeshaji wa fani mbalimbali kama utawala, masoko na uhasibu, mchango ambao unahitajika kwa ajili ya maendeleo na ustawi wa uchumi wa taifa katika nyanja tajwa.

Waziri Mkuu alisema baadhi ya wahitimu watapata ajira lakini si kila mhitimu atapata fursa ya kuajiriwa, hivyo serikali itaendelea kuunga mkono azma yao kama chuo kikuu ya kutoa wahitimu wenye tabia, utashi na uwezo wa kutengeneza kazi na si watafuta kazi tu.

Kuhusu ombi la chuo hicho kuruhusiwa kufanya udahili baada ya kufungiwa, Waziri Mkuu alimwagiza Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Profesa Joyce Ndalichako, kujiridhisha iwapo kimekidhi vigezo kabla ya kukipa kibali cha kufanya hivyo.