Serikali yaanza kufufua General Tyre

01Jun 2019
Cynthia Mwilolezi
ARUSHA
Nipashe
Serikali yaanza kufufua General Tyre

SERIKALI imeanza kukaribisha wawekezaji wa sekta binafsi wanaotaka kufufua kiwanda cha matairi cha General Tyre kilichoko jijini Arusha, kupeleka barua zao na kufanya mazungumzo kwenye Shirika la Maendeleo ya Taifa (NDC).

General Tyre.

Waziri wa viwanda na Biashara, Josephat Kakunda, alisema hayo jana  alipotembelea na kukagua eneo la kiwanda hicho kuwa watapokea barua hizo na mapendekezo ya wawekezaji hadi Agosti mwaka huu na kwamba wako ambao wameshajitokeza kuonyesha nia hiyo.

 

Kufufuliwa kwa kiwanda hicho kutawezesha kupatikana kwa zaidi ya ajira 5,000.

Alisema dhamira ya serikali kufufua viwanda vyote ambavyo vimekufa na hadi Juni mwakani wawe wameanza utaratibu wa kuvifufua na mtu asiyefahamu NDC ilipo aende ofisi za Mkuu wa Mkoa Arusha, atapewa maelekezi sahihi.

Kakunda alisema Tanzania ilikuwa na viwanda 156 kati ya hivyo 88 vinafanya kazi, 68 vina matatizo huku 20 vikiwa vimefutwa katika orodha  kwa sababu ya wamiliki kuuza kwa mtindo wa rejareja.

"Lakini viwanda 48 vilivyobaki kati ya hivyo 16 vimerejeshwa serikalini. Kati ya hivyo, 32 viko tayari katika mchakato wa kuvifufua kwa kushirikiana na sekta binafsi na wale wenye viwanda kama wanafahamu vimekufa na hawana mpango wowote wa kufifufua Serikali tutawanyang'anya ifikapo Juni Mosi, mwaka huu.

Lakini kama wana mpango wa kuvifufua hatuna shida nao, lengo ifikapo Juni, mwakani, tuanze utaratibu wa kuvifufua," alisema.

Alisema kwa viwanda ambavyo vimegeuzwa makanisa Serikali haina shida na taasisi hizo za dini isipokuwa yataomba wamiliki wa viwanda waliowapatia maeneo hayo kuwapatia maeneo mengine ya kanisa.

Aidha alipongeza serikali ya Mkoa wa Arusha kwa kulinda eneo la kiwanda hicho na kuhakikisha halijaharibiwa.

Kakunda alisema kufufuka kwa kiwanda hicho si tu kutasaidia ajira Tanzania pekee bali hata Afrika Mashariki na Kati na nchi za Kusini mwa Afrika.

Kuhusu katazo la mifuko ya plastiki, alisema serikali imeweka mazingira bora ya kuhakikisha wananchi wanapata mifuko mbadala na si iliyokatawa kwa kuongeza  uzalishaji kwenye viwanda 15 vilivyoko nchini.

"Kama jana (juzi) nimetembelea kiwanda cha Hai mkoani Kilimanjaro ambacho kinazalisha mifuko 680,000 kwa siku na pia kuagiza kiwanda cha Mgololo, Iringa kiongeze uzalishaji mara tatu kitakapopata malighafi za kutosha ili wenye viwanda watengeneze zaidi mifuko ya karatasi na mingine," alisema.

Naye Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Mrisho Gambo, alisema serikali mkoani hapa, iko tayari kutoa ushirikiano kwa Serikali katika ufufuaji wa kiwanda hicho na hata ikibidi kukiwapo na uhitaji wa eneo la ziada kwa ajili ya kiwanda itasaidia kupatikana.

Habari Kubwa