Serikali yajipanga kukabiliana bidhaa feki

23Mar 2019
Rahma Suleiman
Zanzibar
Nipashe
Serikali yajipanga kukabiliana bidhaa feki

SERIKALI ya Mapinduzi ya Zanzibar (SMZ), imesema imejipanga kuhakikisha bidhaa zote zinazozalishwa nchini zinakidhi viwango katika soko la ndani na nje kwa ajili ya kuongeza thamani.

Waziri wa Biashara na Viwanda, Amina Salum Ali, picha mtandao

Hayo yalisemwa na Waziri wa Biashara na Viwanda, Amina Salum Ali, katika maadhimisho ya Siku ya Viwango katika bara la Afrika ambazo huadhimishwa kwa mara ya kwanza Zanzibar.

Balozi Amina alisema viwango vya ubora wa bidhaa ndiyo kipaumbele cha serikali katika kufikia malengo ya nchi ya viwanda vya kati hatua ambayo itaifanya Zanzibar kuwa wazalishaji wakubwa na kusafirisha bidhaa hizo nje ya nchi.

Alisema serikali imeanzisha wakala wa viwanda vya kati (Snida) kwa ajili ya kufuatilia kwa karibu wazalishaji wa bidhaa za ndani na kuwapa ujuzi na utaalamu utakaowafanya kuzalisha bidhaa zenye ubora unaokubalika.

Aidha, alisema mikakati ya serikali ni kuwafanya wazalishaji wote wa ndani kufikia viwango bora vya uzalishaji wa bidhaa ambavyo vitakubalika na kuingia katika soko la ndani kwa mafanikio makubwa.

“Niwaombe watendaji wa Shirika la Viwango kuwa waadilifu na kuepukana na vishawishi vya rushwa ambavyo vinaweza kuliangamiza taifa kwa kuruhusu uingizaji wa bidhaa zilizopitwa na wakati,” alisema waziri huyo.

Naye Mkurugenzi wa Shirika la Viwango la Zanzibar (ZBS), Khatib Mwadini, alisema wamejipanga vizuri kuhakikisha wanatekeleza malengo na mikakati ya serikali katika kufikia ubora wa viwango kwa bidhaa zinazozalishwa nchini.

Mwadini alisema tayari wapo katika hatua za kujenga maabara nne ambazo zitakuwa na uwezo wa kutoa vipimo vya bidhaa mbali mbali katika malengo ya kufikia ushindani wa uzalishaji wa bidhaa zitakazohimili soko la ndani na nje.

Aidha, aliwataka wazalishaji wa bidhaa ikiwamo wajasiriamali kufikisha bidhaa zao na kupata ubora wa viwango katika shirika la (ZBS) ili kukubalika katika soko kwa mujibu wa masharti ya nchi za Afrika na Kusini mwa Jangwa la Sahara.

''Shirika la Viwango la Zanzibar limepiga hatua kubwa ikiwamo mikakati ya kujenga maabara nne zenye uwezo wa kupima bidhaa mbalimbali za wazalishaji pamoja na wajasiriamali nchini kwa ajili ya kuingia katika soko,'' alisema.

Habari Kubwa