Serikali yajutia uamuzi kutoa kiwanda chake

09Jan 2019
Mary Mosha
Moshi
Nipashe
Serikali yajutia uamuzi kutoa kiwanda chake

WAZIRI wa Viwanda, Biashara na Uwekezaji, Joseph Kakunda, amesema serikali ilifanya makosa kukipa Chama Kikuu cha Ushirika Mkoa wa Kilimanjaro (KNCU), uendeshaji na umiliki wa kiwanda kidogo cha kukobolewa mpunga cha Kilimanjaro Paddy Hulling Company Ltd.

WAZIRI wa Viwanda, Biashara na Uwekezaji, Joseph Kakunda, picha mtandao

Kutokana na makosa hayo yaliyosababisha kusimama kwa uzalishaji kwa muda wa miaka minne, serikali imetangaza uamuzi wake jana, wa kukitwaa kiwanda hicho kutoka mikononi mwa KNCU na kukirejesha serikalini.

Alitangaza uamuzi huo, baada ya kufanya ukaguzi katika kiwanda hicho cha kukoboa Mpunga cha KPHC kilichoko Moshi Vijijini.

“Hiki kiwanda kimeshindwa kufanya kazi tangu mwaka 2015 hadi sasa, na kweli serikali ilifanya makosa makubwa kukipa KNCU inayohudumia kahawa, isimamie uendeshaji wa zao la mpunga. Hapa tulikosea sana,”alieleza Kakunda.

Kwa mujibu wa waziri huyo, kiwanda hicho kilipaswa kukabidhiwa Chama cha Wakulima wa Mpunga (CHAWAMPU) na si KNCU inayosimamia kahawa.

Baada ya kukiri udhaifu huo, Kakunda alisema serikali ya awamu ya tano chini ya Rais Dk. John Magufuli imeamua kukitwaa kiwanda hicho chini ya miliki ya KNCU na kukirejesha mikononi mwa serikali kuanzia sasa.

“Kiwanda hiki tumekichukua na sasa ni mali ya serikali, ndiye mmiliki sahihi wa kiwanda cha KPHC kwa sasa ambaye atakiangalia na kutafuta mwekezaji mbadala wa kukiendesha mapema mwaka huu, ili kianze tena kufanya kazi,”alisema Waziri Kakunda.

Habari zaidi zimeeleza, KNCU licha ya kushindwa kukiendesha kiwanda hicho, bado inakabiliwa na deni la zaidi ya Sh. milioni 323 ambalo walikopa kwa ajili ya kukiendesha kati ya mwaka 2009/2010.

Kufuatia uamuzi huo wa serikali, baadhi ya wakulima wa mpunga wa vijiji vya Chekereki na Mabogini, akiwamo Ernest Massawe na Mwanahawa Hamisi, wameishukuru serikali kwa hatua iliyofikia ya kukiondoa kiwanda hicho mikononi mwa KNCU na kuahidi kukifufua.

Habari Kubwa