Serikali yakunwa usambazwaji wa zana kilimo

16Sep 2020
Na Mwandishi Wetu
Sumbawanga
Nipashe
Serikali yakunwa usambazwaji wa zana kilimo

WIZARA ya Kilimo imeridhishwa na usambazaji wa mbolea nchini unaofanywa na Kampuni ya Agricom Africa Limited kwa kupeleka vijijini matrekta na zana nyingine za kisasa.

Hayo yamebainishwa na Ofisa Mkuu wa Zana za Kilimo wa wizara hiyo, Godwin Mubi, akisema zana hizo ni bora na zitawasaidia wakulima kuzalisha mazao mengi na kuinua kipato cha mkulima.

Akizungumza kwa niaba ya wizara katika mafunzo yanayoendelea wilayani Kalambo, Mkoa Rukwa,  Mubi, alisema wizara inatambua mchango wa Kampuni ya Agricom katika kuinua na kuboresha kilimo kwa kusambaza zana za kilimo katika maeneo mbalimbali nchini. Mkoa wa Rukwa kwa awamu ya kwanza umetengewa zaidi ya matrekta 17.

Alisema lengo la serikali ni kutumia kilimo kuinua maisha ya wakulima nchini kote, lakini tatizo ni kwamba wakulima wengi wana uelewa mdogo sana juu ya matumizi ya zana bora na uhusiano wa zana hizo katika kuinua uzalishaji wa mazao na uboreshaji wa maisha yao wenyewe.

“Agricom Africa ni moja wa wadau ambao wamekuwa wakiunga mkono juhudi ya wizara na serikali kwa ujumla katika kutekeleza mpango wa kuinua sekta ya kilimo awamu ya pili (ASDP II) kwa kuhakikisha zana za kisasa zinawafikia wakulima na wanajua matumizi yake. Tunawapongeza kwa kazi hii inayofanywa kwa manufaa mapana ya taifa letu,” alisema Mubi.

Mubi alisema mafunzo yanayoendeshwa na kampuni hiyo yataondoa tatizo la uelewa mdogo wa wakulima juu ya matumizi ya zana za kisasa na kuwafanya wapende kutumia zana hizo. Amesema matumizi ya zana bora yataongeza uzalishaji mara tatu juu ya uzalishaji unaotokana na jembe la mkono.

“Takwimu zinaonyesha matumizi ya trekta kwa mkoa wa Rukwa ni asilimia 4 tu na asiliamia zaidi ya 80 wanatumia wanyama kazi na iliyobaki ni jembe la mkono. Hali hii ndio imefanya mafunzo haya yaanzishwe mkoani Rukwa,” alisema Mubi na kuongeza kwamba Tanzania ina hekta 44 milioni zinazofaa kwa kilimo, lakini ni hekta 10.8 milioni tu ndizo zinalimwa kwa sasa.

Mkulima wa Kijiji cha Katete Wilaya ya Kalambo, Monica Mgala, alisema kijiji chao hakina trekta na kusema kwamba kijiji kikipata trekta uzalishaji utaongezeka.

Mkuu wa Ufundi wa Kampuni ya Agricom Africa, Philipo William, aliwahakikishia wakulima kwamba zana zote zilizopangwa zitawafikia kwa wakati katika msimu huu wa kilimo.

“Zaidi ya matrekta 17 yatakabidhiwa kwa vyama vya ushirika mwezi Oktoba na Mkuu wa Mkoa wa Rukwa. Kampuni yetu imejipanga vizuri katika kutoa huduma hiyo muhimu kwa wakulima kwa wakati,” alisema William.

Habari Kubwa