Serikali yaomba ratiba maonyesho China

17Jan 2020
Cynthia Mwilolezi
Arusha
Nipashe
Serikali yaomba ratiba maonyesho China

SERIKALI imeuomba ubalozi wa China kuipatia ratiba za maonyesho ya madini nchini kwao ili wafanyabiashara wakubwa wa madini nchini washiriki ili kutangaza aina za madini yaliyopo nchini.

Balozi wa China nchini, Wang Ke, akiwa ameshika madini ya tanzanite, huku akipata maelezo kutoka kwa Mwenyekiti wa Chama cha Wafanyabiashara wa Madini Tanzania (TAMIDA), Sam Mollel (wa pili kushoto), alipotembelea maonyesho kabla ya mkutano wa balozi huyo na wa Tanzania nchini China na wafanyabiashara wa madini, jijini Arusha juzi. Kushoto ni Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Mrisho Gambo. PICHA: WOINDE SHIZZA

Ombi hilo lilitolewa jana jijini hapa na Naibu Waziri wa Madini, Stanslaus Nyongo, wakati akifunga mkutano wa mabalozi wa China na Tanzania pamoja na wafanyabiashara wa madini ulioandaliwa na Chama cha Wafanyabiashara Wakubwa wa Madini (Tamida).

Naibu Waziri Nyongo alisema wakipata ratiba za maonyesho hayo, itakuwa fursa nzuri kwa wafanyabiashara nchini kutangaza madini yaliopo ambayo mengi hayajulikani japo ni mazuri na ya kipekee.

"Na nyie wafanyabiashara mkipata fursa hiyo tumieni vizuri pamoja na kutafuta soko la uhakika la madini yetu kwa sababu China kuna soko kubwa la madini," alisema.

Pia aliagiza wafanyabiashara wakubwa wa madini nchini walioko kwenye soko la madini mjini Arusha, kuzipandisha hadhi ofisi zao ili kuvutia watalii wengi kuwatembelea na kununua madini yao.

"Ikiwezekana angalieni ofisi jengo la Mfuko wa Hifadhi ya Jamii kwa Watumishi wa Umma (PSSSF), ili ziwe na hadhi ya kuvutia. Watalii wakija hapa watembelee hapo kununua zawadi za kwao," alisema Nyongo.

Alisema kwa kuboresha ofisi kutasaidia kupata fedha za watalii ambazo huishia hotelini na kurudi kwao.

Naye Balozi wa China nchini, Wang Ke, aliahidi kutoa ratiba za maonyesho hayo ili wafanyabiashara wapate fursa za kupata soko la madini.

Alisema China wanatumia sana madini katika vitu mbalimbali, hivyo ni sehemu muhimu kwa soko la uhakika la madini.

Habari Kubwa