Serikali yaombwa kubadili maamuzi

03Aug 2017
Elizaberth Zaya
Dar es salaam
Nipashe
Serikali yaombwa kubadili maamuzi

MTANDAO wa Asasi za Kirai (Policy Forum) umeiomba serikali kufikiria upya uamuzi wake wa kuzinyang'anya mamlaka za serikali za mitaa baadhi ya vyanzo vya mapato.

Aidha, asasi hiyo imeitaka serikali itekeleze kikamilifu nia yake ya kuziimarisha kiutawala, kifedha na kisiasa halmashauri ili ziwe huru kimapato na kimaamuzi.

Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam juzi, mwenyekiti wa kikundi kazi cha serikali za mitaa kutoka asasi za kiraia, Israel Ilunde, alisema kama ambavyo serikali iliazimia katika mpango wa maendeleo wa miaka mitano ni vema serikali ikazisaidia mamlaka hizo ili ziweze kujiendesha.

Alisema kunyang'anywa vyanzo vya mapato kwa mamlaka hizo kutazidhoofisha na pia kutachangia zishindwe kujiendesha.

Alisema ni vema serikali ikapeleka pia ruzuku ya kutosha na kwa wakati kwa serikali za mitaa ili kuziwezesha kutekeleza mipango yake kikamilifu.

Ilunde alisema pamoja na wajibu huo wa serikali, halmashauri nazo zinapaswa kuongeza juhudi za kubuni vyanzo vipya vya mapato yake ya ndani ambavyo havitakuwa kero kwa wananchi ili kuziwezesha kutekeleza mipango yake kwa urahisi.

“Mwaka 2007 Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) ilipewa jukumu la kukusanya mapato ya kodi ya majengo kwenye manispaa za Kinondoni, Ilala na Temeke, lakini utekelezaji wake ulikuwa duni na kurejeshwa kwenye halmashauri husika," alisema Ilunde na kueleza zaidi:

"Kwa hiyo tunaishauri serikali kuwa na msimamo na sera zake, sheria, mipango na miongozo juu ya ukusanyaji wa kodi za majengo.”

Alisema kwa kuwa mpango wa maendeleo wa miaka mitano umejielekeza katika kuongeza mapato ya ndani kutokana na vyanzo vipya pamoja na umuhimu wa kodi ya majengo kama chanzo kikuu cha mapato ndani ya serikali za mitaa, ni vema ikaheshimu hilo na kuziachia mamlaka hizo vyanzo vyake vya mapato.

Alisema serikali za mitaa kuwa na upungufu wa mapato ya ndani kutachangia kufifisha na kuchelewesha utekelezaji wa shughuli zake za maendeleo na kupunguza kasi na ari ya serikali katika kutunza na kuboresha miundombinu katika halmashauri hususani kwa zile zinazotegemea zaidi vyanzo vyake vya ndani.

Habari Kubwa