Serikali yapania kufufua viwanda vya ngozi nchini

21Apr 2016
Na Waandishi Wetu
Mwanza
Nipashe
Serikali yapania kufufua viwanda vya ngozi nchini

SERIKALI ina mpango wa kufufua viwanda vidogo vikiwamo vya kusindika ngozi ili kuinua uchumi wa Taifa kupitia wajasiriamali wanaojishughulisha na shughuli za mazao yatokanayo na ngozi.

Katibu Mkuu Wizara ya Biashara, Viwanda na Uwekezaji, Profesa Adolf Mkenda.

Lengo la hatua hiyo ni kukuza uchumi unaokua kwa kasi kulinganisha na uchumi wa baadhi ya nchi nyingine za Afrika.

Katibu Mkuu Wizara ya Biashara, Viwanda na Uwekezaji, Profesa Adolf Mkenda, aliyasema hayo alipokuwa akifungua mafunzo ya siku tano ya utengenezaji viatu na bidhaa za ngozi kwa wajasiriamali 50 wanaojishugulisha na mazao ya ngozi Kanda ya Ziwa.

“Lengo ni kuwapa elimu itakayowasaidia katika kuandaa, kuzalisha bidhaa bora za ngozi zitakazoshika nafasi katika soko la biashara, mafunzo hayo yaliyosimamiwa na kauli mbiu ‘ngozi ni mali, ngozi ni pesa kwa sasa Watanzania tuna fursa kubwa ya kuuza bidhaa nje bila kodi, hivyo changamkieni fursa," alisema.

Naye Kaimu Mkurugenzi wa Mamlaka ya Maendeleo ya Biashara nchini (Tantrade), Edwin Rutageruka, alisema jukumu kubwa ni kutangaza fursa zilizomo zaidi kwa kuangalia fursa zilizosahaulika.

Rutageruka alisema Serikali ya Awamu ya Tano inayoongozwa na Rais Dk. John Magufuli, imeweka dhamira ya dhati kukuza sekta ya viwanda.

Imeandikwa na Neema Emmanuel na Winfrida Joseph, Mwanza