Serikali yashauriwa kuchukua hatua kunusuru zao la migomba

15Mar 2019
Na Mwandishi Wetu
Mbeya
Nipashe
Serikali yashauriwa kuchukua hatua kunusuru zao la migomba

SERIKALI imeshauriwa kuchukua hatua za haraka kunusuru zao za migomba lililobainika kushambuliwa na kudhoofishwa na minyoo hatari iliyogunduliwa na Taasisi ya Utafiti wa Kilimo Kituo cha Kibaha kilichopo mkoani Pwani.

Taasisi hiyo ilibaini kuwapo kwa minyoo hiyo ambayo hushambulia migomba na kusababisha athari nyingi ikiwamo mimea kubadilika rangi, kuzaa ndizi dhaifu na hatimaye mgomba kuanguka.

Akizungumza jana na Nipashe jijini Mbeya, Mtafiti kutoka Taasisi ya Kilimo, Kituo cha Kibaha, Ambilikile Mwanisongole, alisema wakati wanafanya utafiti walibaini kuwepo kwa aina tatu za minyoo ambayo ni michirizi, Fundo ambazo dalili zake ni kuota vinundu kwenye mzizi wa mgomba.

Mnyoo wa tatu ni Chimba ambao huchimba hadi chini ya mgomba na kusababisha kuoza na kueleza athari za minyoo hiyo kuwa ni mgomba kuanguka.

“Tulifanya utafiti katika mikoa inayolima kwa wingi zao la ndizi na tumebaini kuwapo kwa minyoo ambayo inatishia kudhoofisha zao hilo endapo hatua za haraka hazitachukuliwa kudhibiti kuenea zaidi kwa minyoo hiyo,” alisema Mwanisongole.

Mtafiti kutoka Taasisi ya Kilimo Kituo cha Uyole jijini Mbeya, Daud Mbongo, alisema kutokana na kubainika kwa Minyoo hiyo ya mimea, watafiti na wataalam wa Kilimo kutoka Kituo cha Utafiti wa Kilimo cha Kibaha mkoani Pwani na Kituo cha Utafiti wa Kilimo cha Uyole mkoani Mbeya wameanza kutoa elimu kwa wakulima kuhusu namna ya kudhibiti na kukabiliana na athari za minyoo hiyo.

Alisema baada ya kubaini tatizo hilo wamekuja na suluhu ambapo wakulima walielekezwa namna ya kudhibiti hiyo minyoo ili isiendee kuwapo shambani.

Aliongeza kuwa wakulima ambao mashamba yao bado hayajavamiwa na minyoo hiyo walielekezwa namna ya kukabaliana nayo.

Baadhi ya wakulima wa ndizi kutoka katika Halmashauri za Rungwe, Kyela na Busokelo ambao walipatiwa elimu ya kudhibiti minyoo hiyo katika Kituo cha Ilenge wilayani Rungwe, wamekiri kuona dalili na athari za minyoo hiyo kwenye mashamba yao.

Walisema licha ya kuona dalili na athari za minyoo hiyo kwenye migomba lakini hawakuelewa chanzo cha dalili hizo mpaka walipoanza kupewa elimu kuhusiana na minyoo hiyo.

Habari Kubwa