Serikali yataja mikakati mitano usafiri majini

23May 2020
Augusta Njoji
Dodoma
Nipashe
Serikali yataja mikakati mitano usafiri majini

IKIWA ni miaka 24 tangu kutokea kwa ajali ya Mv. Bukoba, serikali imetaja mikakati mitano iliyochukuliwa ili kuimarisha usalama katika usafiri wa majini nchini.

Ajali hiyo ilitokea Mei 21, mwaka 1996,  watu takribani 800 walipoteza maisha katika Ziwa Victoria na meli hiyo ilikuwa ikitokea Bukoba kwenda Mwanza na kuzama maeneo ya Bwiru.

Akizungumza jana na waandishi wa habari jijini hapa, Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Isack Kamwelwe, alisema serikali imeboresha usafiri kwa njia ya maji katika maziwa makuu kwa kufanya miradi mbalimbali.

Alitaja miradi hiyo kuwa ni ukarabati wa meli mbili katika Ziwa Victoria ambazo ni Mv. Victoria na Mv. Butiama, ujenzi wa chelezo na ujenzi wa meli mpya kubwa katika Bandari ya Mwanza Kusini.

“Kwa kuwa tumekarabati meli na kujenga mpya katika ziwa lile lile iliyotokea ajali ya Mv. Bukoba, nimeona leo niwajulishe wananchi jinsi serikali ilivyojipanga kuhakikisha inarejesha usafiri katika ziwa hili,”alisema.

Vile vile, alisema tangu kutokea kwa ajali hiyo serikali imejizatiti na kuchukua hatua mbalimbali za kuimarisha usalama wa usafiri wa majini.

Alisema mkakati mwingine ni uboreshwaji wa Sheria na Mamlaka ya Udhibiti wa Usafiri wa Majini huku ikiimarisha usimamizi wa usalama wa usafiri majini kwa kuweka Ofisi na wakaguzi wa meli wa Shirika la Wakala wa Meli Tanzania (Tasac) kwenye mikoa yote inayopakana na maziwa makuu.

“Ukaguzi huu unahakikisha kuwa meli zote zinazofanya safari majini zina vifaa vya kujiokolea vinavyotosheleza idadi ya watu waliomo kwenye chombo na abiria kupewa maelekezo ya kutumia vifaa hivyo,” alisema.

Waziri Kamwelwe alitaja mkakati wa tatu ni kuboresha shughuli za utafutaji na uokoaji na kuanzisha kituo cha uokoaji na utafutaji cha Dar es Salaam.

“Serikali kwa kushirikiana na Shirika la Bahari Duniani (IMO), imejenga kituo cha kuratibu shughuli za utafutaji na uokoaji katika Bandari ya Dar es Salaam na kinasimamiwa na Tasac, kinafanya kazi saa 24 na siku saba za wiki,” alisema.

Akizungumzia mkakati wa nne wa miundombinu ya bandari, Kamwelwe alisema serikali imeendelea kuimarisha miundombinu ya Bandari katika Maziwa Makuu na Bahari ya Hindi ili kuwa salama na zenye ufanisi zaidi.

“Mkakati wa tano ni uboreshaji wa mafunzo na utoaji wa vyeti vya mabaharia, serikali imeimarisha usimamizi wake chini ya Chuo cha Bahari Dar es salaam (DMI), kwa mujibu wa Itifaki ya Kimataifa na vyeti vinatambuliwa kimataifa na mabaharia wa Tanzania watafanya kazi meli yoyote duniani,”alisema.

Habari Kubwa