Serikali yataka umakini katika usalama chakula

08Oct 2017
Beatrice Shayo
Nipashe Jumapili
Serikali yataka umakini katika usalama chakula

SERIKALI imesema chakula kilichoko kwenye hifadhi kimepungua ikilinganishwa na mwaka jana na kwamba kunahitajika umakini, ili kuwapo na uhakika wa chakula nchini.

Waziri wa Kilimo, Mifugo na Uvuvi, Dk. Charles Tizeba.

Aidha, serikali imesema haijapiga marufuku kusafirishwa kwa nafaka nje ya nchi, bali kinachotakiwa ni kwa mazao hayo kuongezwa thamani kabla ya kusafirishwa.

Hayo yalisemwa juzi jijini Dar es Salaam na Waziri wa Kilimo, Mifugo na Uvuvi, Dk. Charles Tizeba, wakati alipokuwa akifungua kongamano la saba la Baraza la Nafaka Afrika Mashariki (EACB).

Alisema wamekamilisha tathmini ya upatikanaji wa chakula nchini na kwa mavuno yaliyopo, kuna ziada ya chini ikilinganishwa na mwaka jana ambayo ilikuwa asilimia 123 huku mwaka huu kilichopo kikiwa ni asilimia 120.

“Maana yake tusipokuwa na uangalifu kidogo tutaserereka kwenye upungufu wa chakula nchini. Kwa hiyo pamoja na hilo, tunasema wafanyabiashara waendelee kufanya biashara, lakini serikali ijue. Sina uhakika kama kuna nchi duniani inaruhusu chakula kutoka bila serikali kujua kinachotoka,” alisema.

Aidha, alisema mkakati wa Tanzania ni kujenga viwanda kwa ajili ya uchumi wa wa kati wenye lengo la maendeleo ya viwanda ambao unatokana na malighafi za kilimo ndiyo maana wanashawishi umma na wafanyabiashara kuongeza thamani mazao kabla ya kupeleka kwenye masoko ya nje ya nchi.

Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi wa Baraza la Nafaka Afrika Mashariki (EACB), Eugene Rwibasira, alisema uhitaji wa chakula katika Bara la Afrika unaendelea kuongezeka na soko la chakula katika nchi za Afrika linatarajiwa kufikia dola za Marekani trilioni 1 ifikapo mwaka 2030. Kiwango cha sasa ni dola bilioni 300.