Serikali yatoa neno  ulipaji kodi utalii

15Jan 2018
Cynthia Mwilolezi
Nipashe
Serikali yatoa neno  ulipaji kodi utalii

NAIBU Waziri wa Fedha na Mipango, Dk. Ashatu Kijaji, amesema Serikali haifurahishwi na ulipaji kodi kwa baadhi ya wadau wa sekta ya utalii na madini kwa kuwa wapo ‘wanaoipiga’ serikali kwa kukwepa kodi stahiki.

Alisema hayo wakati akizungumza na wafanyabiashara ya utalii na madini jijini hapa, mwishoni mwa wiki.

Alitaka wafanyabiashara na hasa wa madini na utalii kulipa kodi ili kuharakisha uchumi wa viwanda.

“Katika hili la kodi hakuna namna mtu atakwepa, ni lazima mlipe kodi na kwa kutumia mfumo wa mashine za kielekroniki (EFDs) ili kukwepa kumpa mtu fedha mkononi na kutoa mianya ya rushwa,” alisema.

Alisema maendeleo ya taifa lolote duniani ni mapato, kwa kuwa bila mapato hakuna uhai wa taifa.

Alisema endapo kila mtu atalipa kodi bila kusukumwa, Tanzania itakuwa na uchumi mzuri zaidi ya sasa katika nchi za Afrika Mashariki na kuwa mfano.

“Tutaangalia jinsi ya kukaa pamoja na kundi hili ili tuzungumze wanatupiga eneo lipi.

“Tunataka twende pamoja, hata ikibidi, tusaidie nchi maskini kuliko sisi, uwezo huo tunao,” alisema.

Aliwataka maofisa wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) kuacha kukaa ofisini, badala yake wazungukie wafanyabiashara wajionee changamoto walizonazo.

“Nyie TRA acheni kujiona wakubwa kuliko Watanzania wengine, wote ni sawa hakuna aliye zaidi ya mwingine katika serikali hii,” alisema.

Nae Mwenyekiti wa Chama cha Waongoza Watalii Tanzania (Tato), Willy Chambulo, aliomba serikali kupunguza mrundikano wa kodi zinazokusanywa na mamlaka mbalimbali na badala yake zikusanywe na TRA pekee.

“Jamani sio TRA, Mamlaka ya Chakula na  Dawa (TFDA), Wakala wa Usalama na Afya Mahali pa Kazi (OSHA),  Zima Moto wote hawa wanakusanya kwetu kodi kubwa, wekeni kodi katika kapu moja na mfumo uwe wa mtandao wa ulipaji, mtagawana huko kuliko sisi kuhangaika na wote hawa na kwa mtindo huu fedha lazima ivuje maana wapo wajanja wanapiga,” alisema.

Hata hivyo, alidai sekta ya utalii na madini wanajitahidi kukusanya kodi bila kusukumwa lakini kama wapo wachache wanaowaharibia jina ni vema wakae pamoja na serikali wawekwe sawa.

  

 

 

Habari Kubwa